Habari Mseto

Afisa wa DCI asukumwa jela miaka 5 kwa utekaji nyara

November 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

AFISA mmoja wa polisi Ijumaa alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani kwa hatia ya kuwateka nyara raia wawili wa Ethiopia miaka sita iliyopita na kuwarudisha kwao akidai walikuwa nchini Kenya kwa nia ya kushambulia nchi hii kwa bomu.

Hakimu mkuu Mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi alimsukumia Inspekta Painito Bera Ng’ang’ai kifungo hicho baada ya kumpata na hatia katika mashtaka matano.

Bw Andayi alimpata na hatia Ng’ang’ai ya kuwateka nyara Ali Ahmed Hussein na Sulub Abdi Ahmed na kuwasafirisha hadi Ethiopia kupitia kituo cha mpakani cha Moyale kaunti ya Marsabit bila idhini yao.

Insp Ng’ang’ai alikuwa anahudumu katika kitengo cha uchunguzi wa jinai (DCI) eneo la Kilimani alipowateka nyara Ali na Sulub mnamo Januari 26, 2014.

Akipitisha hukumu, Bw Andayi alimtoza Insp Ng’ang’ai faini Sh600,000 ama kifungo cha miaka miwili gerezani.

Kwa kosa la kutumia mamlaka ya polisi vibaya alipowateka nyara Ali na Sulub mshtakiwa alitozwa faini ya Sh400,000 ama atumikie kifungo cha miaka miwili.

Kwa kosa la kudanganya alitozwa faini ya Sh100,000 ama kifungo cha mwaka mmoja.

“Vifungo vitaambatana. Ikiwa utaweza kulipa faini ya Sh1.1milioni utatoka jela na ukishindwa utatumika jumla ya miezi 60 gerezani,” aliamuru Bw Andayi alipomuhukumu mshtakiwa.

Bw Andayi alisema mshtakiwa alitumia vibaya mamlaka ya polisi badala ya “kutenda haki akitumikia kila mmoja anayeishi nchini Kenya kama kauli mbiu ya polisi –utumishi kwa wote.”

“Ili iwe funzo kwa maafisa wengine wa polisi wasirudi kutumia mamlaka yao vibaya utumikia vifungo hivyo kimoja baada ya kingine,” aliamuru Bw Andayi.

Ali na Sulub ambao ni wanachama wa kundi la waasi la Ogaden nchini Ethiopia walikuwa wamefika humu nchini kufanya mashauri ya kutafuta suluhu ya mzozo kati waasi hao na Serikali ya Ethiopia.

Walikamatwa wakiwa nje mkahawa eneo la Kilimani Nairobi na kuingizwa ndani ya gari aina ya Toyota Prado KBS 533S na kusafirishwa hadi mjini Moyale kaunti ya Marsabit na kuingizwa nchini Ethiopia bila idhini yao.

Wawili hao walikuwa wamefika nchini Kenya kwa mwaliko wa kufanya mashauri ya kutafuta suluhu ya mzozo kati ya Serikali ya Ethiopia na waasi hao wa Ogaden.

Akipitisha hukumu Bw Andayi alisema mashahidi 21 waliofika mbele yake walithibitisha Ng’ang’ai alitekeleza uhalifu huo akishirikiana na watu wengine watatu walioachiliwa akiwamo afisa mwingine wa Polisi.

Alimpa mshtakiwa siku 14 kukata rufaa.