• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Pasta auawa kwa tuhuma za wizi wa nyeti za wanaume

Pasta auawa kwa tuhuma za wizi wa nyeti za wanaume

Na AFP

DAUDU, Nigeria

AMRI ya kutotoka nje imetengazwa sehemu kadha za jimbo la Benue kufuatia kisa ambapo pasta mmoja aliuawa na umma kwa madai ya kuiba nyeti za mwanaume, maafisa walisema.

Visa vya wizi wa “sehemu za siri za wanaume” ambapo nyeti za waathiriwa huamini kuwa huzama mwilini, vinasemekana kukithiri zaidi nchini Nigeria na nchi kadha za Afrika Magharibi. Aghalabu hali kama hii imechochea machafuko katika jamii ambapo watu wanaoshukiwa kuchangia maajabu kama hayo hushambuliwa na halaiki.

Kisa cha hivi punde kilitokea katika mji wa Daudu, ulioko umbali wa kilomita 250 kutoka mji mkuu wa Abuja.

Maafisa wa serikali walisema kuwa kundi moja la vijana lilituhumu pasta huyo na mshirika wake mwingine kwa kuhusika na kitendo hicho cha kinyama.

Hata hivyo, Mkuu wa Serikali za Wilaya Caleb Aba alikataa tuhuma hizo akisema: “Ilithibitishwa kuwa madai hayo hayakuwa ya kweli kwani uchunguzi wa kisayasi ulifaywa.”

Mshirika wa pasta huyo alizuiliwa na maafisa wa usalama kama njia ya kumlinda dhidi ya kushambuliwa.

Naye pasta huyo, kwa kuhofia maisha yake, aligura mji huo, kulingana na msemaji wa polisi Cathrine Anene. Aliongeza kuwa kanisa lake liliteketezwa na vijana wenye hasira baada yake kutoweka.

“Lakini vijana walimfuata pasta huyo na kumuua. Hatimaye tulipataa mwili wake,” msemaji huyo akaongeza.

Bw Aba alisema kwamba baada ya siku mbili vijana hao pia walimtuhumu mtu mwingine kwa kosa la kuondoa nyeti za kijana mmoja.

“Mwanamume huyo alipigwa hadi akazirai kabla ya polisi kuingilia kati,” Aba akasema, akielezea sababu ya kutangazwa kwa kafyu hiyo.

Wanajeshi na maafisa wa polisi waliletwa katika eneo hilo kulinda doria baada ya vyombo vya habari kuripotiwa kuwa kundi moja la vijana lilivamia soko likiimba,“bila nyeti hakuna soko”. Vurugu hizo zilisambaratisha shughuli za kibiashara katika mji wa Daudu.

Watu wanane walikamatwa kwa kusabisha kuvuruga utulivu na kuchochea ghasia, polisi wakasema.

Maafisa walisema kafyu ambayo iliwekwa mnamo Jumatatu itadumu hadi hali ya usalama iimarike.

You can share this post!

Serikali yamkata pembe Magoha kwa kumdhulumu afisa wizarani

Elijah Manangoi naye pia apigwa marufuku kwa kutumia pufya