Kazi yangu si kufurahisha watu, asema Maraga
Na RUTH MBULA
JAJI Mkuu David Maraga ambaye amekuwa akilaumiwa na wanasiasa na maafisa wa serikali kwa misimamo na maamuzi yake, amesema kuwa kazi yake si kufurahisha watu.
Bw Maraga ambaye ataastafu mwaka ujao, alisema kwamba kamwe hajuti kwa maamuzi aliyofanya akitekeleza kazi yake.
“Iwapo nitajaribu kufurahisha watu, sitatekeleza haki. Sisi kama majaji tunaamua kesi kwa kutegemea ushahidi unaowasilishwa kwetu na kwa kuzingatia sheria. Hivyo ndivyo haki na Maandiko Matakatifu ya Mungu yanavyotuhitaji kufanya. Kufurahisha watu sio kutenda haki,” Bw Maraga alisema alipofungua mahakama ya Borabu katika Kaunti ya Nyamira alikozaliwa.
Akiwa Jaji Mkuu, Bw Maraga ametofautiana na Rais Uhuru Kenyatta kufuatia maamuzi yake hasa pale mahakama ya juu ilipofuta matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2017 ambao alikuwa ametangazwa mshindi.
Rais Kenyatta pia amekuwa akilaumu mahakama kwa kuhujumu ajenda za serikali yake.Naye Bw Maraga amemlaumu Rais Kenyatta kwa kukataa kuapisha majaji 41 waliopendekezwa na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC).
Vile vile amekuwa akilaumu wabunge kwa kupunguza bajeti ya mahakama na amependekeza bunge ivunje kwa kukosa kupitisha sheria ya kuhakikisha usawa wa jinsia.