Habari Mseto

MKU yapata ufadhili

November 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

KITENGO cha sayansi katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimepokea ufadhili kutoka chuo kimoja cha nje kwa ajili ya kuhifadhi msitu wa Brackenhurst mjini Limuru, Kenya.

Ufadhili huo umepatikana kupitia ushirikiano wa chuo cha Nottingham Trent University (NTU), na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Ufadhili huo wa Erasmus Plus Grant ni wa kufikia Sh110 milioni ambzo zitatumika kwa matumizi tofauti katika msitu wa Brackenhurst, mjini Limuru, kwa uhifadhi wake na kuulinda kutokana na ubora wake kwa maswala mengine.

Wakati huo utahifadhiwa ili kujua ubora wa mchanga wake na maswala ya uhifadhi wa chakula katika mazao.

Kulingana na mpangilio uliopo Dkt Charles Warui atakuwa akishughulika katika ulinzi kuhusu msitu huo.

Msitu wa Brackenhurst mjini Limuru, Kenya. Picha/ Hisani

Ufadhili huo pia ni muhimu kwa sababu utanufaisha wanafunzi wa chuoni na wale wanaendesha somo la uzamili.

Wanafunzi kumi na wanachama sita katika vitengo sita tofauti watanufaika pakubwa na ufadhili huo wa Erasmus Plus Grant, kutoka chuo cha NTU huku chuo cha MKU kikishirikiana kwa ubadilishaji wa wanafunzi kuenda kujifunza mengi katika vyuo vikuu vingine vya nje.

Dkt Mary Muriuki ndiye aliteuliwa kuongoza maswala ya utafiti katika somo la sayansi.

“Ninapongeza MKU kwa kupata nafasi ya kuteua wanafunzi wachache ambao watazamia katika utafiti kutokana na ufadhili huo,” alisema Dkt Muriuki.

Alisema msitu huo wa Limuru hautanufaisha chuo hicho pekee lakini hata wakazi wa eneo hilo watapata manufaa.

“Utafiti huo utaleta mwelekeo mpya kwa sababu utaleta ufahamu wa kulinda na kuutunza udongo na mabadiliko ya tabianchi,” alisema msomi huyo.

Alitoa changamoto kwa wanafunzi popote walipo wawe mstari wa mbele kujihusisha na utafiti kwa sababu huo ndio mwelekeo wa masomo ya siku za usoni.