• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Hofu chanjo ya corona huenda isifikie nchi za Afrika mapema

Hofu chanjo ya corona huenda isifikie nchi za Afrika mapema

Na AFP

PARIS, UFARANSA

MATAIFA maskini yakiwemo ya Afrika, yamo hatarini kukosa chanjo za kukinga maradhi ya Covid-19 mapema.

Nchi nyingi tajiri tayari zimeagiza mabilioni ya dozi za chanjo hizo, lakini wataalamu wanahofia mataifa maskini yataachwa nyuma.

Kando na umaskini unaoathiri uwezo wa kushindania chanjo hizo mapema, imebainika ni chanjo zinazohitaji miundomsingi ya kisasa kuhifadhiwa.

Ingawa nchi tajiri zimepanga kumaliza zoezi la kuwapa chanjo raia wake kufikia mwishoni mwa mwaka ujao, wataalamu wanaonya kuwa nchi maskini zinakabiliwa na changamoto ya raia wake kufikiwa mara tu chanjo itakapoidhinishwa kuwa salama kwa matumizi na taasisi husika.

Kampuni za Pfizer na BioNTech zinapanga kutoa chanjo hizo mara tu baada ya kupata kibali cha matumizi yake kutoka kwa mamlaka za kuhalalisha matumizi ya dawa.

Zinatarajia kutoa dozi 1.3 bilioni kufikia mwaka 2021.

Matokeo ya duru ya tatu ya majaribio yalionyesha kwamba chanjo aina ya mRNA inafaa kwa kiwango cha asilimia 90 katika kudhibiti athari za virusi vya corona.

Chanjo pia haikuonyesha madhara yoyote mabaya kwa maelfu ya watu ambao walijitokeza ili kufanyiwa majaribio.

Kiwastani, gharama ya matibabu yanayojumuisha chanjo hiyo inakisiwa kuwa Sh4,000. Mataifa tajiri tayari yameagiza mamilioni ya dozi za chanjo hizo. Kufikia sasa, bado haijabainika kiwango ambacho nchi maskini zitapata.

“Ikiwa tutakuwa na chanjo ya kampuni ya Pfizer na kila mtu atahitaji dozi mbili, basi hiyo ni changamoto kubwa inayotuandama,” akasema Trudie Lang, ambaye ndiye mkurugenzi wa Mpango wa Afya Duniani katika Chuo Kikuu cha Oxford.

Mnamo Aprili, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilibuni mpango maalum uitwao COVAX kuhakikisha kwamba nchi zote duniani zitafaidika chanjo dhidi ya virusi hivyo itakapopatikana.

Mpango huo unazishirikisha serikali za nchi mbalimbali, wanasayansi, mashirika yasiyo ya serikali na sekta ya binafsi. Hata hivyo, kampuni ya Pfizer si mshiriki wa mpango huo.

Msemaji mmoja wa kampuni hiyo alisema “imeeleza nia ya kutaka kusambaza chanjo hizo kwa wale wote waliojumuishwa kwenye mpango huo.”

Rachel Silverman, ambaye ni mtaalamu kuhusu sera katika Kituo cha Maendeleo Duniani, alisema huenda nchi maskini zikakosa kufikiwa na chanjo zitakazotolewa katika awamu ya kwanza.

Alisema tayari dozi 1.1 bilioni zishaagizwa na nchi matajiri, hali inayoifanya vigumu kwa nchi hizo kufikiwa.

“Kwa mwelekeo kama huo, huenda wengine wasipate,” akasema.

Baadhi ya nchi ambazo tayari zimeagiza chanjo kama Japan na Uingereza ni washiriki wa COVAX.

Inatarajiwa huenda nchi maskini zikazitegemea nchi tajiri kufikiwa na chanjo kupitia makubaliano mbalimbali ya ununuzi.

Amerika imeagiza dozi 600 milioni japo si mwanachama wa COVAX.

You can share this post!

Waiguru hatarini kufungiwa nyumba

AK yatenga Sh500,000 kwa washindi wa mbio za Mountain...