Kemsa kuna PPE za kutosha kuzuia wahudumu wa afya kuambukizwa corona – Kagwe
Na SAMMY WAWERU
WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe amesema kuna vifaa vingi vya kutumia kujikinga – PPE – katika ghala la Shirika la Kusambaza Dawa na Vifaa vya Kimatibabu (Kemsa) ambavyo wahudumu wa afya wanafaa kutumia wakati huu wa janga la Covid-19.
Akitetea jitihada za serikali katika kupambana na virusi vya corona, Bw Kagwe amesema mdahalo wa ‘kutokuwepo kwa vifaa vya kimatibabu’ umechochewa kwa msingi wa kisiasa.
Waziri alisema wanaoeneza uvumi wa kutowepo kwa PPE na vifaa vingine kukinga maambukizi ya corona miongoni mwa madaktari na wahudumu wengine wa afya, wana ajenda zao binafsi na zisizopaswa kujumuishwa katika oparesheni kupambana na ugonjwa huu ambao ni janga la kimataifa.
Wahudumu wa afya, wakiongozwa na Muungano wa Madaktari, Wataalamu wa Dawa na Madaktari wa Meno (KMPDU), wamekuwa wakilalamikia upungufu na ukosefu wa PPE na vifaa vingine muhimu katika kuhudumia wagonjwa wa corona.
Wanasema mengi ya maafa ya madaktari na wahudumu wa afya yaliyosababishwa na Covid-19, pamoja na maambukizi yamechangiwa na ukosefu wa vifaa kujikinga.
Bw Kagwe hata hivyo, Jumatano usiku kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, alisisitiza kwamba Kenya ina vifaa vya kutosha.
“Tuna vifaa vingi sana, vikiwemo PPE katika ghala la KEMSA. Ni vingi hata kupita kiasi,” akasema Kagwe.
Alieleza ni vingi kiasi kwamba viwanda na watengenezaji wa vifaa hivyo wanaviuza nje ya nchi.
“Serikali za kaunti ziviendee KEMSA,” Bw Kagwe akahimiza.
Kauli ya Waziri inajiri wakati ambapo Kemsa imezongwa na madai ya sakata za ufisadi na utoaji wa zabuni kwa njia isiyofaa.