• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Sh17B zahitajika kuajiri walimu

Sh17B zahitajika kuajiri walimu

Na FAITH NYAMAI

TUME ya Huduma ya Walimu (TSC), imefichua kwamba, inahitaji Sh17 bilioni kuajiri walimu zaidi ya 12,000 ili kukabiliana na upungufu shule zitakapofunguliwa Januari.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Nancy Macharia alisema kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na shule za upili, kuna uhaba wa walimu 26,804. Alisema kwa sababu ya kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona shuleni ambapo madarasa yataongezwa, kutakuwa na uhaba wa walimu shuleni.

Shule zitakapofunguliwa Januari wanafunzi watawekwa katika makundi madogo kuwaepusha kusongamana madarasani, hatua ambayo itahitaji walimu wengi kuwashughulikia.

Katika shule nyingi za umma, kila darasa linafaa kuwa na wanafunzi 40 lakini kuna zilizo na wanafunzi zaidi ya 60. Kufuatia mpango wa kugawa wanafunzi wa darasa la 25 kila darasa, walimu watakuwa na kazi nyingi zaidi. Bi Macharia alisema tume inapanga kuajiri walimu 12,626 kila mwaka kutua uhaba uliopo na utakaotokana na hali hii mpya.

Alisema kufikia sasa, tume hiyo imewaajiri walimu 23,700 pekee tangu 2017 badala ya walimu 50,504 ilivyopanga.

“Tume ilikuwa imepanga kuajiri walimu 12,500 kila mwaka katika miaka mitano ijayo kupunguza tatizo la uhaba wa walimu nchini. Hata hivyo, lengo hili halijatimizwa kutokana na uhaba wa fedha,” akasema.

Kulingana na ripoti ya tume hiyo ya mwaka huu wa kifedha, ilipokea Sh2.5 bilioni za kuajiri walimu 5,000.

Vile vile, chini ya mpango wa kupunguza makali ya janga la corona kwa uchumi, TSC ilitengewa Sh2.4 bilioni za kuajiri walimu 12,000 vibarua.

Kulingana na Mwenyekiti wa TSC, ambaye muda wake wa kuhudumu ulitamatika Jumatano, Dkt Lydia Nzomo, kabla ya wizara ya elimu kuanzia kutekeleza mpango wa kuhakikisha wanafunzi wote wanajiunga na shule za upili, kulikuwa na uhaba wa walimu 61, 671 katika shule za upili.

Kenya inahitaji walimu 50,504 (12,626 kila mwaka) kufanikisha mpango huo.

Kuanzia mwaka wa kifedha wa 2017/2018 na 2019/2020, serikali iliajiri walimu 18,700 ili kutimiza mpango huo wa kuhakikisha wanafunzi wote wanaofanya mtihani wa darasa la nane (KCPE) wanajiunga na kidato cha kwanza.

Hali hiyo ilisababisha uhaba wa walimu katika shule za upili kuwa 80,849.

“Uhaba wa walimu wa shule za msingi katika kipindi hicho pia umepungua kutoka 40,807 hadi 36,777 mwaka huu,” alisema.

Bi Macharia alisema tume inahitaji Sh1 bilioni kuwaandaa walimu kwa ufunguzi wa shule kupitia mafunzo.

Alisema kufikia sasa, walimu 45,703 wamepatiwa mafunzo.

You can share this post!

BI TAIFA OKTOBA 10, 2020

BI TAIFA OKTOBA 11, 2020