Madiwani wadai ipo njama mpya ya kumtimua Sonko
Na COLLINS OMULO
BAADHI ya madiwani katika Kaunti ya Nairobi wanadai kwamba kuna njama za kufufua upya juhudi za kumng’oa mamlakani Gavana Mike Sonko, kwa kukataa kuidhinisha bajeti ya Kaunti hiyo.
Madiwani hao kutoka mirengo yote ya kisiasa walisema tayari, mpango umebuniwa kuwasilisha hoja ya kumng’oa mamlakani.
Madiwani hao walidai kuwa kuna mkutano uliofanyika katika afisi za Capitol Hill, Nairobi, ulioshirikisha uongozi wa Bunge la Kaunti hiyo, ambapo lengo lake kuu ni kuweka mkakati kuhusu vile mchakato huo utakavyofufuliwa upya.
Katika siku za hivi karibuni, Bw Sonko amekuwa akimkosoa vikali Rais Uhuru Kenyatta kuhusu hatua mbalimbali anazochukua.
Miongoni mwa masuala ambayo amejitokeza kuyakosoa ni ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) na kujumuishwa kwa Halmashauri ya Huduma za Jiji (NMS) katika usimamizi wa baadhi ya huduma jijini.
Tofauti kali pia zimeibuka kati ya gavana na madiwani wengi, baada yake kukataa kuidhinisha bajeti hiyo ya Sh37.5 bilioni, ambayo iliitengea NMS Sh27.1 bilioni na kuacha serikali ya Kaunti na Sh8.4 bilioni pekee.
Ukusanyaji saini
Diwani Peter Warutere wa wadi ya Roysambu, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Sonko, alidai mkutano uliofanyika Capitol Hill, uliitishwa kujadili jinsi kiongozi huyo atakavyong’olewa mamlakani.
Alidai mipango ipo tayari ili kuanzisha juhudi za kukusanya saini za kuunga mkono hoja hiyo.
Hata hivyo, alisema mpango huo hautafaulu kwani hawataweka saini zao.
“Ninatoa hakikisho kuwa kama madiwani wa Jubilee, hatutaunga mkono Gavana Sonko kung’olewa mamlakani. Yeye ni gavana wetu. Ikiwa kuna suala lolote linamhusu, tunaweza tu kufuata maagizo tunayopewa na Rais Kenyatta,” akasema Bw Warutere.
Diwani wa wadi ya Highrise, Bw Kennedy Oyugi, alisema kuwa mpango huo ulijadiliwa na kuungwa mkono na uongozi wa vyama vya Jubilee na ODM kwenye bunge hilo.
Alisema moja ya sehemu ya mpango huo ni kumrejesha Bw Edward Gichana kama Karani wa Bunge kabla ya hoja hiyo kuwasilishwa. Alisema hoja imepangiwa kuwasilishwa bungeni kabla ya mwisho wa mwezi huu.
“Mkutano ulishirikisha uongozi wa vyama hivyo viwili kuangazia mpango huo,” akasema Bw Oyugi.
Duru zilieleza hoja hiyo ilipangiwa kuwasilishwa wiki iliyopita, lakini wanaoiendesha wakakosa kukubaliana kuhusu utaratibu utakaozingatiwa.
Jaribio kama hilo lilifanyika Februari lakini likazimwa baada ya Rais Kenyatta kuingilia kati.
Kiongozi wa Wachache kwenye bunge hilo, Bw Michael Ogada, alikubali uwepo wa mkutano huo lakini akakana mpango wa kumng’oa mamlakani Bw Sonko kuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa.
Badala yake, alisema mkutano uliitishwa kujadili mkakati wa kukusanya saini kuunga mkono mchakato wa BBI.
Vile vile, mkutano uliitishwa kuhakikisha bunge limezungumza kwa sauti moja kuhusu mpango huo.
“Ni kweli tulifanya mkutano katika afisi ya Capitol Hill. Ni mkutano ulioushirikisha uongozi wote wa bunge. Ajenda kuu ilikuwa suala la ripoti ya BBI, kuhakikisha kwamba hakuna migawanyiko inayoibuka,” akasema.
Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Naibu Kiongozi wa Wachache, Bw Moses Ogeto.