• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
BBI: Bondeni kwagawanyika

BBI: Bondeni kwagawanyika

EVANS KIPKURA na ONYANGO K’ONYANGO

SIASA za ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) zinaendelea kuwagawanya viongozi wa Bonde la Ufa huku hisia za mseto zikitolewa kuhusu namna mchakato wa ukusanyaji wa saini milioni moja utaendelezwa eneo hilo.

Bonde la Ufa ni ngome ya kisiasa ya Naibu Rais Dkt William Ruto ambaye anapinga ripoti hiyo akisisitiza kuwa haijajumuisha matakwa ya Wakenya wote.

Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos ambaye anaunga mkono BBI, amewataja wanaoipinga kama watu wasiojielewa na wana nia ya kudhihirisha tu uaminifu wao kwa Dkt Ruto ili kujizolea umaarufu wa kisiasa.

Bw Tolgos ameapa kwamba ataendesha shughuli za ukusanyaji wa saini za BBI eneo hilo, akisema huwezi kuipinga ilhali inaongezea Kaunti ya Elgeyo Marakwet Sh3 milioni kwenye mgao wake wa kifedha kila mwaka.

“Inakuaje kiongozi hasa anayetoka Elgeyo Marakwet apinge pendekezo ambalo litaongezea kaunti hii Sh3 milioni? Huo ni ubinafsi na mapuuza makubwa hata kama ni kudhihirisha uaminifu wa kisiasa kwa kiongozi fulani,” akasema Gavana huyo.

Bw Tolgos alishikilia kuwa ukusanyaji wa saini utaendelea Bonde la Ufa jinsi ulivyoratibiwa licha ya baadhi ya viongozi kuapa kutoruhusu shughuli hiyo katika maeneo yao.

Gavana wa Nandi Stephen Sang’ ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto alinukuliwa kwenye hafla moja akiapa kuwa hataruhusu saini za BBI zikusanywe katika kaunti yake.

“Matamshi yaliyotolewa na gavana wa Nandi kwamba atasambaratisha ukusanyaji wa saini za BBI hayafai kutoka kwa kiongozi wa hadhi yake. Nataka kumwambia kuwa hata apinge kivipi, wananchi wa Nandi bado watakuwa na nafasi ya kutia saini zao kwenye stakabadhi za BBI,” akaongeza Bw Tolgos.

Bw Sang’ alinukuliwa akiwataka Wakenya wanaotaka kutia saini za kuidhinisha BBI waende kaunti nyingine kwa kuwa hakuna wanaounga mkono ripoti hiyo kutoka Nandi.

Hata hivyo, Bw Tolgos alisisitiza kwamba atahakikisha Wakenya kutoka kaunti ambazo wananchi watatishiwa dhidi ya kusaini BBI eneo la Bonde la Ufa wafanye hivyo katika magatuzi jirani.

Mwenyekiti wa ODM katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet Micah Kigen hata hivyo alisema kaunti hiyo ipo tayari kwa shughuli ya kutia saini zao na kuiunga mkono BBI.

“Kukataa BBI nzima haifai kutokana na masuala machache ndani ya ripoti hiyo. Tunafaa tuzungumzie marekebisho yanayohitajika badala ya kukataa BBI yote,” akasema Bw Kigen.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei naye amewataka madiwani eneo la Bonde la Ufa wajiepushe na mchakato wowote wa kupitisha BBI, akisema ripoti hiyo inatumiwa na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na kinara wa ODM Raila Odinga kuendeleza ajenda zao za kisiasa.

“Madiwani wasikubali watumiwe kupitisha stakabadhi ambayo ina nia ya kuwagawanya Wakenya. Kwa nini viongozi wa bonde la Ufa waliachwa nje kwenye hafla ya uzinduzi wa saini?” akauliza seneta huyo.

You can share this post!

Korti yazima jaribio la kushtaki Matiang’i

Moto wateketeza mali ya thamani kubwa Githurai