• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Moto wateketeza mali ya thamani kubwa Githurai

Moto wateketeza mali ya thamani kubwa Githurai

Na SAMMY WAWERU

WAFANYABIASHARA wa vifaa vya mbao Githurai wanakadiria hasara kubwa baada ya moto kuteketeza mali yao Ijumaa.

Chanzo cha moto huo ulioanza mwendo wa saa saba mchana hakijabainika kufikia sasa.

Eneo lililoathirika pakubwa ni lenye makarakana ya mbao na mashine ya kuzipasua.

Ndimi za moto ulioenea kwa kasi pia ziliathiri baadhi ya vifaa vilivyotengenezwa kama vile sofa seti, meza na vinginevyo.

Licha ya vifaa kadha kuokolewa, athari za mkasa zilitishia watumizi wa Thika Road na kusababisha msongamano wa magari.

Wazima moto kutoka Kaunti ya Nairobi kwa ushirikiano na maafisa wa kijeshi (KDF) kitengo cha zimamoto, waliitika na iliwachukua muda wa saa nne mfululizo kuuzima.

“Tumepoteza mali ya mamilioni ya pesa kufuatia mkasa huu,” akasema Bw Muiruri, mmoja wa wafanyabiashara wa mbao.

Huku idara ya polisi ikianzisha uchunguzi, baadhi ya wafanyabiashara wanadai huenda moto huo ulisababishwa na hitilafu za nguvu za umeme, wengine wakishuku ulianzishwa kimakusudi.

“Si mara ya kwanza moto kutokea eneo hili, kuna siasa potovu zinazochezwa hapa na tunaomba serikali iingilie kati na kunasa wenye nia ya kutuhangaisha,” akasema mfanyabiashara, akikadiria hasara kubwa.

Seneta maalum, Isaac Mwaura ni kati ya viongozi waliofika eneo la mkasa ‘kufariji’ walioathirika.

You can share this post!

BBI: Bondeni kwagawanyika

Familia ya Safari Rally yaomboleza kifo cha Nagin Chouhan