• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Uingereza sasa yaidhinisha matumizi chanjo ya corona

Uingereza sasa yaidhinisha matumizi chanjo ya corona

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

UINGEREZA Jumatano iliibuka nchi ya kwanza duniani kuidhinisha matumizi ya chanjo ya kampuni ya Pfizer-BioNTech kukabili virusi vya corona.

Taifa hilo lilisema chanjo hiyo itaanza kutolewa kwa raia wake kuanzia wiki ijayo.

“Serikali leo imekubali pendekezo kutoka kwa Mamlaka ya Kuidhinisha Matumizi ya Bidhaa za Matibabu (MHRA) kuidhinisha chanjo kutoka kwa kampuni ya Pfizer-BioNTech kwa matumizi dhidi ya virusi vya corona,” ikasema serikali kwenye taarifa.

“Chanjo hiyo itaanza kutolewa kote nchini kuanzia wiki ijayo,” ikaongeza.

Waziri wa Afya, Matt Hancock, alisema kuwa mpango huo utaanza mapema wiki ijayo.

“Hizi ni habari njema sana,” akasema Hancock.

Kamati maalum ya kusimamia taratibu za utoaji chanjo nchini humo itaamua makundi ambayo yatapewa chanjo hiyo kwanza.

Baadhi ya wale wanaotarajiwa kufaidika kwanza ni watu wanaowahudumia wagonjwa majumbani mwao, wahudumu wa afya na wazee, kwani ndio wako kwenye hatari zaidi kuambukizwa virusi.

Kufikia sasa, taifa hilo limethibitisha visa 1.6 milioni tangu Machi, huku watu zaidi ya 59,000 wakifariki, kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali.

Kampuni ya Pfizer kutoka Amerika, mshirika wake BioNTech kutoka Ujerumani na ile ya Moderna kutoka Amerika zimetangaza tafiti za awali zimeonyesha chanjo hiyo inafaa kwa kiwango cha asilimia 90.

Pfizer ilisifia hatua ya Uingereza kuidhinisha chanjo yake, ikitaja hilo kama tukio la kihistoria kwenye vita dhidi ya janga hilo.

“Kuidhinishwa kwa chanjo ni hatua ambayo tumekuwa tukilenga kuifikia, tulipotangaza kwanza ni kupitia utafiti pekee ambapo ushindi dhidi ya janga hili ungepatikana. Tunasifia sana hatua ya MHRA kutathmini umahsusi wa chanjo yetu na kuchukua hatua ya haraka kuwalinda raia wa Uingereza dhidi ya athari za corona,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Albert Bourla.

“Tunapoendelea kutarajia nchi nyingi kuidhinisha matumizi yake, tutadumisha ubora wa chanjo hiyo katika maeneo yote tutakayoagizwa kupeleka kote duniani,” akasema.

Kando na Uingereza, Amerika na Muungano wa Ulaya (EU) pia zinatathmini umahsusi wa chanjo hiyo.

Pfizer ilisema itaanza kusafirisha viwango vidogo vidogo vya chanjo nchini Uingereza, huku ikiendelea kungoja ikiwa Mamlaka ya Kusimamia Dawa na Vyakula (FDA), Amerika, itaidhinisha matumizi yake.

Mamlaka inatarajiwa kutoa uamuzi huo mapema wiki ijayo.

You can share this post!

Karata ya Naibu Rais kusukuma refarenda 2022

Nzige wavamia mashamba na malisho Lamu