Je, wewe ni mbunifu? Google imetoa Sh200 milioni kushindaniwa
Na BERNARDINE MUTANU
Kampuni ya Google imezindua hazina ya kufadhili biashara zisizo za kujifaidisha ya Sh200 milioni.
Ufadhili huo utawanufaisha washindi 12 katika shindano la African Google Impact Challenge na unatolewa kwa lengo la kuifaa jamii
“Tunaamini kuwa teknolojia inaweza kusaidia mashirika ya humu nchini na yale ya kimataifa kutimiza malengo na kusuluhisha baadhi ya changamto zinazoshuhudiwa Afrika,” alisema meneja wa Google nchini Charles Murito.
Kampuni hiyo inawafadhili wale wanaojihusisha na masuala ya teknolojia na wale watakaokuwa na athari kubwa na nzuri kwa jamii.
Watakaoshiriki shindano hilo wana miezi sita ya kutuma ombi kuzingatiwa, kabla ya pendekezo kuchunguzwa na washindi kuamuliwa.
Washindi wa kwanza wanne watapokea Sh25 milioni na wengine nane watapokea Sh12.5 milioni.
Umma pia umepewa nafasi ya kupigia kura pendekezo ambalo wanahisi linavutia zaidi, lililo na athari njema zaidi na ambalo utekelezaji unawezekana.
Majaji watakuwa Manu Chandaria, Caroline Mutoko, Tegla Loroupe, Tabitha Karanja, Janet Mawiyoo, Salim Mohammed na Charles Murito.