Familia ya mwanamume aliyepata ulemavu mikononi mwa wanaosemekana kuwa ni maafisa wa polisi yadai haki
Na MISHI GONGO
FAMILIA moja mjini Mombasa inadai haki baada ya jamaa wao Bw Joseph Macharia kupata ulemavu kupitia kipigo alichopata kutoka kwa watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi.
Bw Macharia mwenye umri wa miaka 35, anadaiwa kupokea kipigo kutoka kwa maafisa wa kutekeleza masharti ya kafyu mnamo Mei 23, 2020.
Kulingana na mamake kijana huyo Bi Rose Waruguru, mwanawe alikuwa ameenda dukani aliposimamishwa na maafisa wa polisi waliokuwa wakipiga doria.
“Alitoka saa chache kabla kafyu kuenda dukani, lakini hakurudi. Alfajiri siku ya pili nilipokea simu kutoka kwa jirani yangu kuwa walimuokoa mtoto wangu akiwa hali mahututi ambapo alinieleza kuwa kwa kuhofia wao pia kupokea kichapo waliamua kumueka ndani kwao hadi asubuhi,” akasema Bi Waruguru.
Bi Waruguru alisema miezi saba tangu tukio hilo mwanawe amepoteza fahamu na inamlazimu aache kazi alizokuwa akifanya kumpatia riziki ili kumhudumia mwanawe.
“Nilikuwa nafanya vibarua vya kufua lakini kutokana na hali ya kiafya ya mwanangu, nimelazimika kusitisha kazi hizo. Japo anatumia dawa hajapata afueni, hana uwezo wa kuzungumza, kujigeuza, kusikia na hata kufumbua macho ni tatizo. Chakula tunampa kutumia mirija,” akasema.
Alieleza kuwa walimpeleka katika hospitali ya Port Reitz ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu na nusu lakini hakupata nafuu.
“Baada ya kufanyiwa uchunguzi madaktari walibaini kuwa alipigwa kichwa jambo lililomfanya kupata uvumbe. Madaktari waliniamuru kurudi nyumbani baada ya miezi mitatu mtoto wangu akiwa bado hajapata afueni. Nilipowauliza waliniambia niendelee kumpa dawa na kuwa inaweza kuchukua muda mrefu kabla ya kijana wangu kurudisha uwezo wa kujihudumia,” akasema.
Kulingana na Bi Waruguru kijana wake ambaye ni mkazi wa Eldoret alikuwa amekuja kumsalimia lakini akaathiriwa na marufuku ya kuwazuia watu kusafiri kutoka au kuingia kwa baadhi ya kaunti.
“Kijana wangu na familia yake walikuwa wakiishi Eldoret japo walitengana na mkewe. Alikuwa akifanya kazi ya ufudi wa magari kabla kupata ajali hii,”akasema.
Alieleza kuwa japo alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha changamwe na hata kuripoti katika Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi (IPOA) hajapata usaidizi wowote.
Kwa sasa anaomba Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kuingilia kati ili kijana wake apate haki.
Mama huyo pia anawaomba wahisani kumpa usaidizi wa chakula na fedha akisema kuwa tangu kuzorota kwa hali ya kiafya ya mwanawe alilazimika kuacha vibarua alivyokuwa akifanya kujipatia riziki.
“Nilikuwa nafulia watu kujikimu kimaisha lakini kwa sasa nimelazimika kuacha. Kupata chakula na kulipa kodi imekuwa changamoto kwangu; nadaiwa kodi ya miezi saba na chakula nategemea wahisani. Serikali haijanipa ufadhili wowote,”akasema.
Alisema japo shirika la IMLU linasimamia matibabu ya mwanawe, kumpatia lishe bora kijana huyo imekuwa changamoto.
Afisa wa shirika la kutetea haki za kibinadamu MUHURI Bw Francis Auma alishutumu maafisa wa polisi katika maeneo ya Changamwe, Chaani, na Jomvu kwa kutumia nguvu kupita kiasi kuwakumbusha wakazi kuzingatia masharti ya kujikinga kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.
Alidai kuwa wiki mbili zilizopita maafisa wa polisi eneo la Jomvu walimsukuma mwanamume mmoja kwa jina Hassan Roble kutoka kwa gari, kitendo kilichosababisha yeye kupoteza uhai.
“Mafisa wa polisi wanazidi kuwaumiza raia kutokana na serikali kuwalinda. Katika eneo hili tumerekodi visa vingi vya watu kupoteza maisha na hata kupata vilema mikononi mwa polisi na hao maafisa wa polisi wanaendeleza uovu huo kwa kuwa kesi dhidi yao hupelekwa hivi na vile na baadaye wanaondolewa hatiani,” akasema.