• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Ruto akataa kuungana waziwazi na kambi ya ‘La’

Ruto akataa kuungana waziwazi na kambi ya ‘La’

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amesema hana haja kushiriki mashindano kuhusu mageuzi ya Katiba kupitia kura ya maamuzi kwani mashindano hayo yataathiri juhudi za kukabiliana Covid-19 miongoni mwa changamoto zinazowasibu Wakenya.

Dkt Ruto Jumapili, Desemba 6, 2020, alisema Katiba ni ya Wakenya wote na haifai kutumiwa kuwagawanya kupitia makundi ya “NDIO” na “LA”.

Alisema njia ya kipekee ya kuendeleza mpango wa kuunganisha Wakenya kipindi hiki kigumu ni kuhakikisha kuwa mpango wa mageuzi wa Katiba unashirikisha Wakenya wote.

“Hizi ni nyakati ngumu. Mataifa mbalimbali yako mbioni kusaka chanjo dhidi ya Covid-19. Kwa hivyo, huu sio wakati wa kuwaweka Wakenya katika makundi ya NDIO na LA. Hii kura ya maamuzi ikamilishwe haraka ili Wakenya waendelee na shughuli za kupambana na changamoto zingine zinazowakabili,” akasema alipohudhuria Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Jesus Is Alive Ministries (JIAM) eneobunge la Starehe, Kaunti ya Nairobi.

“Hatuko tayari kwa mashindano; wale wanaotutisha kwa kututaka tujiunge na mrengo wa LA wanapoteza wakati wao,” Dkt Ruto akaongeza.

Naibu Rais alikariri kuwa inafaa Wakenya waruhusiwe kupigia kura masuala mbalimbali wakati wa kura ya maamuzi badala ya kupiga kwa marekebisho yaliyopendekezwa mara moja.

“Ikiwa Wakenya wanaweza kupiga kura kuchagua washikilizi wa viti sita katika uchaguzi mkuu, ninaamini kuwa wanaweza kufuata mtindo huo huo katika kura ya maamuzi ya kuwa kupigia kura vipengele mbalimbali,” Dkt Ruto akasema.

Aliandamana na wabunge George Theuri (Embakasi Magharibi), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), na Sylvanus Osoro ( Mugirango Kusini). Wengine walikuwa Maseneta Susan Kihika (Nakuru), Aaron Cheruiyot (Kericho), na Millicent Omanga (Seneta Maalum).

You can share this post!

COVID-19: Kenya yafikisha visa jumla 88,380 idadi ya vifo...

Wakenya Jepchirchir na Chebet washinda Valencia Marathon