Afueni madaktari wakiahirisha mgomo kwa siku 14
Na CHARLES WASONGA
WAKENYA wamepata afueni japo kwa muda baada ya madaktari kusimamisha mgomo wao kutoa nafasi kwa mazungumzo zaidi kuhusiana na masilahi yao.
Kwenye taarifa kilichotuma kwa vyombo vya habari Jumapili jioni, Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) kilisema kimechukua hatua hiyo baada ya serikali, bunge la kitaifa na seneti kuomba muda zaidi wa mazungumzo.
“Tumeamua kusimamisha kwa muda mgomo wetu kwa muda wa siku 14 kwa kutambua juhudi za mabunge mawili ya kitaifa katika kutatua malalamishi tuliyoibua kwenye notisi ya mgomo tuliyoitoa Novemba 16, 2020,” akasema kaimu Katibu Mkuu wa KMPDU Chibanzi Mwachonda kwenye taarifa hiyo.
Akaongeza: “Tunatambua nia nzuri ya madaktari wa Kenya na umma. KMPDU inatarajia kukutana na Kamati za Afya katika Bunge la Kitaifa na Seneti mnamo Desemba 9 na Desemba 10.”
KMPDU ilikuwa imeitisha kuanza mgomo Jumatatu, Desemba 7, 2020, kulalamikia ukosefu wa vifaa vya kujikinga (PPE) hospitalini, marupurupu ya kufanya kazi katika mazingira hatari na bima ya afya kwa wanachama wake walio katika mstari wa mbele kupambana na janga la Covid-19.
Hata hivyo, kwenye taarifa ya kusimamisha mgomo huo, Dkt Mwachonda alibainisha kuwa madaktari watarejelea mgomo wao Desemba 21, 2020, ikiwa matakwa yao hayatakuwa yametimzwa.
Hata hivyo, Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) na kile cha maafisa wa Kliniki vimeshikilia kuwa mgomo wao utaanza Jumanne, Desemba 8, 2020, wakilalamikia mahitaji hayo hayo ya madaktari.
Kufikia Jumatatu, zaidi ya wahudumu wa afya 30, wakiwemo madaktari 10 wataalamu katika fani mbalimbali za matibabu, wamefariki baada ya kuugua Covid-19 tangu Aprili 2020.