DPP kukata rufaa dhidi ya kuachiliwa kwa bwanyenye Humphrey Kariuki
Na RICHARD MUNGUTI
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) atakata rufaa kupinga uamuzi wa kuachilia huru kwa bwanyenye Humphrey Kariuki katika kesi ya ukwepaji kulipa ushuru wa Sh7.4 milioni.
Mnamo Jumatano hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot alitupilia mbali kesi ya kutolipa ushuru wa Sh7.4m ya mapipa 80 ya kemikali ya Ethanol yaliyokutwa katika viwanda vya Africa Spirits Limited (ASL) na Wow Beverages Limited (WBL).
Pia Bw Kariuki alikuwa ameshtakiwa kwa kutolipa ushuru wa Sh5.8m wa Ethanol hiyo.
Bw Cheruiyot alisema sababu ya kumwachilia Bw Kariuki ni kwa sababu DPP alikosa kuwasilisha ushahidi katika kesi hiyo.
Mahakama ilisema kuwa kwa muda wa miezi 16, DPP alishindwa kuwasilisha ushahidi na kwamba sheria inamtaka DPP awasilishe ushahidi bila kuchelewa.
Ijapokuwa Bw Kariuki aliachiliwa katika kesi hiyo bado kungali na kesi nyingine za kutolipa ushuru wa Sh41bn na pia kupatikana na risiti feki za ushuru wa forodha.
Kesi hizo mbili zinasikizwa na mahakimu wakuu Bw Francis Andayi na Bi Martha Mutuku.
Bw Kariuki alishtakiwa pamoja na wakurugenzi wa makampuni ya ASL na WBL Mabw Peter Njenga ,Robert Thinji Mureithi, Eric Mulwa Nzomba na Bw Kefa Gakure.
Bw Cheruiyot alisema DPP alikaidi kifungu nambari 50(2)(e) cha katiba kinachomtaka akamilishe kesi katika muda usio mrefu.
Mawakili Kioko Kilukumi, Cecil Miller na Philip Murgor walisema kucheleweshwa kusikizwa kwa kesi hizo ni ukandamizaji wa haki za washtakiwa.
DPP alikuwa ameomba korti iahirishe kwa muda usio julikana kesi hiyo ndipo aunganishe kesi tatu zinazomkabili Bw Kariuki na wenzake.
Mahakama iliamuru washtakiwa warudishiwe dhamana ya pesa tasilimu Sh11milioni kila mmoja aliyokuwa amelipa ndipo wafanye kesi wakitoka nyumbani.