Habari Mseto

CHAGUZI NDOGO: Hakuna kupiga kura bila barakoa

December 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imewaonya wapigakura watakaoshiriki katika chaguzi ndogo zitakazofanyika Jumanne kwamba hawataruhusiwa katika vituo vya kupigia kura bila kuvalia barakoa.

Kamishna Buya Molu, Jumatatu aliwaambia wanahabari katika makao makuu ya tume hiyo, Nairobi, kwamba masharti mengine kama kudumisha umbali wa mita moja na nusu au zaidi na watu kunawa mikono na kutumia sanitaiza yatazingatiwa.

Alisema masharti ya Covid-19 yatakazingatiwa katika chaguzi hizo ndogo ziliandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na zimesambazwa kwa maafisa wote wa uchaguzi katika ngazi za wadi na maeneobunge.

“Tutakuwa na afisa atakayekuwa na kifaa cha kupima joto (thermos gun) kila kila kituo cha kupigia kura. Pia kutakuwa na maeneo ya kunawa mikono au kutumia vieuzi kando na kwamba maafisa wote wa uchaguzi watakuwa na barakoa na glavu. Kwa hivyo, tunawaomba wapigakura kuzingatia masharti yote haswa uvaliaji wa barakoa,” Bw Molu akasema.

“Hakuna atakayeruhusiwa kupiga kura katika kituo chochote ikiwa hatakuwa amevalia barakoa,” akasisitiza.

Kauli hiyo ya Molu inajiri mwezi mmoja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kwamba watu wasiovalia barokoa wasipewe huduma popote pale.

Chaguzi ndogo zitafanyika Jumanne katika eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale na wadi za Kahawa-Wendani (Kiambu), Kisumu Kaskazini (Kisumu), Lake View (Nakuru), Dabaso (Kilifi) na Wundanyi/Mbale katika kaunti ya Taita Taveta.

Kiti cha ubunge cha Msambweni kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge Suleiman Dori alishinda kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa 2017 kwa tiketi ya ODM. Dori alifariki mnamo Machi 26, 2020.

Wagombeaji wakuu katika kinyang’anyiro hicho ni Omar Boga (ODM), Feisal Bader (mgombeaji huru) anayeungwa mkono na Naibu Rais William Ruto na Sheikh Abdurahman Mahmoud wa chama cha Wiper.

Wengine ni Marere Wamwachai (National Vision Party), Hassan Mwakulonda (Party of Economic Democracy) na wagombeaji huru wengine, Charles Bilal na Mansour Kumaka.

Wagombeaji hao wote wanang’ang’ania jumla ya wapiga kura 68,621 waliosajili wa katika wadi za Gombato/Bongwe, Ukunda, Kinondo na Ramisi.