• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Mbunge wa Thika aitaka serikali iwe chonjo chanjo ya Covid-19 ‘isitupite’

Mbunge wa Thika aitaka serikali iwe chonjo chanjo ya Covid-19 ‘isitupite’

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya inastahili kutoa msimamo wazi jinsi itakavyoagiza chanjo ya CoviD-19 kutoka nchi za ng’ambo.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema chanjo hiyo ni muhimu kwa wananchi wa Kenya ili kukabiliana na maradhi hayo.

“Tunaelewa ya kwamba kwa wakati huu nchi nyingi zinajizatiti kuona ya kwamba zinaagiza kwa wingi chanjo hiyo ili kuokoa maisha ya raia wao ambao pia wameathirika kutokana na Covid-19,” alisema Bw Wainaina.

Alisema ni muhimu wakuu serikalini kujipanga ili ifike nchini ama 2021 au 2022.

“Kwa hivyo ni jambo la busara kuanza kujipanga mapema kupitia Wizara ya Afya. Wale wanaohusika wanastahili kuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba chanjo hiyo imeagizwa mara moja,” alisema mbunge huyo.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi mjini Thika katika afisi ya NG-CDF alipohutubia waandishi wa habari.

Alipendekeza kuwa iwapo chanjo hiyo itafika hapa nchini watu wa kwanza wanaostahili kupata chanjo hiyo wawe ni madaktari na wahudumu wote wa afya, wazee, halafu wengine wafuatiye baadaye.

“Nilazima tujaribu kupanga maswala hayo kulingana na umuhimu wake kwa sasa. Homa hiyo imeathiri watu wengi nchini bila kusaza hata wahudumu wote wa afya,” alisema Bw Wainaina.

Alitoa mwito kwa watu wanaosafiri mashambani kuwa makini wanapojumuika na wapendwa wao hasa wakongwe ambao ndio wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa corona.

You can share this post!

Mawaziri wapewa likizo ya Krismasi na Mwaka Mpya

COVID-19: Visa vipya 390