• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Maandamano yachacha Sudan kushinikiza mageuzi

Maandamano yachacha Sudan kushinikiza mageuzi

Na MASHIRIKA

KHARTOUM, Sudan

RAIA nchini Sudan walifanya maandamano makubwa wikendi, wakiitaka serikali ya mpito nchini humo kuharakisha mageuzi ya kidemokrasia.

Maandamano hayo, yaliyofanyika Jumamosi, yaliadhimisha miaka miwili tangu jeshi kumwondoa mamlakani aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Omar el-Bashir.

Maandamano yalijiri huku taharuki ikiendelea kuwepo kati ya wanajeshi na viongozi wa kiraia katika serikali hiyo, ambayo ilibuniwa baada ya Bashir kukamatwa Aprili mwaka uliopita.

Serikali hiyo imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha utekelezaji wa mipango ya mageuzi kama ilivyokubaliwa.

Waandamanaji walichoma magurudumu ya magari katika wilaya ya Al-Sahafa, iliyo kusini mwa mji mkuu, Khartoum, huku wakielekea katika afisi za rais wakisema: “Tunataka haki.”

Wengi wao, ambao ni vijana, walisema hawajaona mabadiliko yoyote nchini humo, kwani inaendelea kukumbwa na changamoto za kiuchumi.

Walibeba bendera ya taifa hilo na picha za watu ambao waliuawa kwenye maandamano ya awali.

“Kupitia maandamano haya, leo tumetoa ujumbe maalum kwa serikali ya mpito. Tuna nguvu kama raia. Ndiyo silaha yetu. Tutaitumia ikiwa matakwa yetu hayatatimizwa,” akasema Nada Nasereldine, mwenye umri wa miaka 21.

Maandamano kama hayo pia yalifanyika katika miji ya Omdurman, Bahri, Madani, Atbara, Kassala na Port Sudan. Inakisiwa maelfu ya watu walishiriki kwenye maandamano hayo kuonyesha kutoridhika kwao na uongozi wa serikali hiyo.

Katika Uwanja Mkuu wa Ndege wa Khartoum, waandamanaji walibeba mabango yenye picha ya Waziri Mkuu, Abdalla Hamdock wakikashifu uongozi wake.

“Enda kabisa!” wakasema baadhi yao.

“Raia wanataka utawala huu kubadilishwa,” wakaeleza.

Jumbe kama hizo zilishuhudiwa kwenye maasi yaliyofanyika katika nchi kadhaa za Arabuni miaka kumi iliyopita.

“Tumeamua kuandamana kwa sababu serikali ya mpito haitaki kusikia wala kutimiza haja yetu,” akasema Hani Hassan, 23, ambaye alikuwa miongoni mwao.

Kama wenzake, alisema serikali haijali kuhusu hali ya kiuchumi, inayondelea kudorora kila kuchao.

Bashir aliondolewa mamlakani na wanajeshi mwaka uliopita, ambapo sasa amefunguliwa mashtaka kuhusu mapinduzi yakijeshi ya 1989, aliyotatumia kutwaa uongozi.

Vile vile, anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kibinadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), nchini Uholanzi.

Hata hivyo, wale waliohusika katika mauaji ya waandamanaji kati ya 2018-2019 bado hawajachukuliwa hatua zozote za kisheria.

Serikali hiyo inakabiliwa na kibarua kigumu kuimarisha hali ya uchumi, kutimiza matakwa ya waandamanaji na kutatua suala la ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana.

Serikali hiyo pia imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kufadhili bajeti kutokana na uhaba mkubwa wa fedha.

You can share this post!

Celtic wanyanyua ufalme wa Scottish Cup kwa mara ya 40

Raila atakuwa rais wa tano wa Kenya – Wabunge