Habari Mseto

COVID-19: Visa vipya 349 vyafikisha 94,500 idadi jumla

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

IDADI ya watu ambao sampuli zao zimepimwa nchini kubaini ikiwa wameambukizwa virusi vya corona au la sasa imepita milioni moja.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe Jumapili kuhusu hali ya Covid-19 nchini, idadi jumla ya vipimo imetimu 1,008,518.

Vile vile, visa vilivyothibitishwa vya maambukizi viligonga 94,500 baada ya watu 349 zaidi kupatikana na virusi vya corona.

Hii ni kutokana na sampuli kutoka kwa watu 5,025 zilizopimwa ndani ya kipindi cha saa 24.

Waziri Kagwe alisema kuwa wagonjwa sita zaidi wamefariki kutokana na Covid-19 na hivyo kufikisha 1,639 idadi jumla ya wale ambao wamefariki kwa sababu ya ugonjwa huu nchini Kenya.

“Na wakati huu kuna wagonjwa 831 waliolazwa katika vituo mbalimbali vya afya kote nchini huku wengine 5,834 wakiuguzwa nyumbani,” akasema kwenye taarifa hiyo aliyoituma kwa vyombo vya habari.

Bw Kagwe aliongeza kuwa wagojwa 52 wa Covid-19 wamelazwa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU), 25 wanasaidiwa kupumua kwa matumizi ya mitambo maalum (ventilators) na 24 wanaongezwa hewa ya oksijeni.

Nairobi inaongoza kwa maambukizi mapya kwa kuandikisha visa vipya 156, Nyeri (34), Kirinyaga (30), Meru (27), Uasin Gishu (25), Mombasa (17), Kiambu (15), Busia (13) huku Nandi ikiwa na visa saba.

Nayo kaunti ya Murang’a imenakili visa sita, Nyandarua (4), Machakos (3), Garissa (2), Kisii (2), Trans Nzoia (2) huku kaunti za Tharaka Nithi Turkana, Kajiado, Nakuru, Embu na Laikipia zikiandikisha kisa kimoja kila moja.