MARY WANGARI: Viongozi wa kike waheshimiwe, taasubi za kiume zikome
NA MARY WANGARI
KATIKA sehemu kubwa ya wiki iliyopita, Wakenya waliachwa vinywa wazi wakati wanasiasa walipoonekana kutupilia mbali urazini wao na kuvuana nguo hadharani.
Uchaguzi mdogo katika eneo la Mswambweni, Kaunti ya Kwale, uligeuka upesi uga wa fujo na ubabe wa kijinsia.Cheche za matusi ya soni baina ya Msemaji wa Chama cha ODM Edwin Sifuna na Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, Mwanaharakati Boniface Mwangi na Seneta Mteule Millicent Omanga, ziliwaacha baadhi ya watu wakitafuta pa kuficha nyuso zao kwa fedheha.
Wanaume husika walijitahidi kuwadhalilisha wanawake kwa misingi ya kijinsia na kimaumbile huku wanawake wakiwakabili vilivyo kwa maneno makali.
Inatamausha kwamba katika karne hii ya maendeleo kiteknolojia na mawasiliano, taasubi za kiume zingali zimekolea katika jamii.Hali kwamba baadhi ya wanaume licha ya kiwango cha umri, elimu au hadhi, wangali wanatumia uke kama silaha ya kumdhalilisha na kumweka chini mwanamke ni ithbati tosha kwamba bado tuna mwendo mrefu.
Japo matamshi ya wanawake husika pia yalikuwa ya kufedhehesha ikizingatiwa nafasi yao kama viongozi na zaidi kina mama na wake za watu, hatuwezi kuendelea kupuuza athari ya taasubi ya kiume.
Siasa ni mchezo mchafu, hata hivyo, si sababu tosha ya kuruhusu taasubi ya kiume kuendelea kutumika kama silaha dhidi ya viongozi wa kike au wanawake wanaodhubutu kuwania vyeo na nafasi za uongozi.
Haya yanajiri wakati Kenya inapojitahidi kuongeza idadi ya wanawake uongozini kuhusiana na Kanuni ya Ujumuishaji katika Katiba 2010.
Safari ya kuwezesha ujumuishaji wa kijinsia uongozini imekuwa ndefu na yenye misukosuko tele hasa katika jamii ambayo bado inatawaliwa pakubwa na kasumba potovu.
Kuanzia hadhi ya ndoa, maumbile, mavazi na kadhalika ni baadhi tu ya vigezo vinavyotumiwa kumhukumu mwanamke yeyote anayediriki kujitosa katika siasa.
Endapo mwanamke ni mrembo atapuuziliwa mbali kama aliyepata uongozi au cheo kwa kutumia mwili wake naye yule ambaye si mrembo kulingana na viwango vya kijamii, maumbile yake yatatumiwa na wanaume na hata wanawake wenzake kama silaha ya kumvunja moyo.
Si ajabu kwamba kwa mwanamke kuwa kiongozi Kenya ni sharti awe jasiri na anayejitahidi maradufu zaidi ya viongozi wenzake wa kiume.
Ni sharti kama jamii tusonge na majira na kukubali ujumuishaji wa kijinsia katika tasnia ya siasa ili kufanikisha maendeleo kijamii na kiuchumi.
Ni kawaida kwa viongozi, wake kwa waume, kutofautiana maadamu itakuwa unafiki wa hali ya juu kutarajia waafikiane kwa kila jambo.Hata hivyo, inapaswa kuwa kwa misingi ya kimtazamo, fikra na ajenda anuai wala si kwa misingi ya kijinsia wala maumbile.