Polisi kuimarisha doria sherehe za Krismasi
Na HILARY KIMUYU
POLISI wataimarisha usalama katika sehemu mbalimbali kote nchini, Wakenya wanapojitayarisha kusherehekea sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya chini ya kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Jana, Inspekta Jenerali wa Polisi, Hilary Mutyambai (pichani) alisema kuwa, polisi wamepewa maagizo makali kuhakikisha hakuna yeyote anayekiuka masharti hayo hata kidogo.
“Tutahakikisha masharti hayo yametekelezwa kikamilifu, ikiwemo uzingatiaji wa saa za kafyu. Kuanzia saa nne usiku, kila mmoja anapaswa kuwa nyumbani kwake,” akasema.
Bw Mutyambai alikuwa akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi jana, akiandamana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama Barabarani (NTSA), Bw George Njau na kamishna wa Idara ya Magereza Kenya (KPS), Bw Wycliffe Ogalo.Bw Ogalo alisema idara hiyo itawatuma baadhi ya maafisa wake kuwasaidia polisi kutekeleza masharti hayo.
“Usalama huanzia na mtu binafsi. Hivyo, ninawaomba maafisa wote wa usalama kushirikiana na wananchi. Nawaomba wananchi kutoa maelezo yote watakayokuwa nayo, ambayo yatatusaidia kuzuia vitendo vya uhalifu,” akasema.
Bw Njau aliwaomba polisi kuchukulia hatua magari ya uchukuzi wa umma (PSVs) ambayo yatapatikana yamewabeba abiria wengi kupita kiasi.
Aliwaonya wananchi dhidi ya kuabiri gari lolote ambalo litakuwa likikiuka masharti ya Wizara ya Afya, kwa kuwabeba abiria kupita kiasi.
“Kutakuwa na misako ya ghafla, hasa kwenye barabara kuu. Ili kuepuka kuchukuliwa hatua, tunawaomba madereva na abiria kuzingatia sheria zote za trafiki, kwa mfano kutowabeba abiria kupita kiasi, magari kutokuwa na mikanda ya usalama, madereva kuendesha magari wakiwa walevi kati ya mengine,” akasema.
Hayo yalijiri huku takwimu zikionyesha kuwa watu 3,663 walipoteza maisha yao mwaka huu kutokana na ajali za barabarani.Idadi hiyo ni ongezeko la watu 155, ikilinganishwa na mwaka uliopita, ambapo watu 3, 508 walifariki kutokana na ajali hizo.