Wakenya wengi wana matumaini ya 2021 kuwa bora – Ripoti
Na CHARLES WASONGA
WAKENYA saba kati ya kumi wanahisi kuwa hali ya uchumi ni mbaya kuliko ilivyokuwa msimu wa Krismasi mwaka jana.Hii inaashiria kuwa sherehe za Krismasi mwaka huu hazitakuwa na msisimko na mbwembwe za kukata na shoka kama miaka ya nyuma.
Kulingana na utafiti wa kampuni ya Tifa Kenya, Kenya inakabiliwa na hali hii ngumu kutokana na janga la Covid-19. Wale walielezea kuathirika zaidi na athari za corona ni wakazi wa Nairobi.
Lakini nusu ya idadi jumla ya Wakenya wako na matumaini kwamba hali yao ya kiuchumi itaimarika 2021, huku asilimia 25 wakihisi kuwa hali itakuwa mbaya zaidi.
Wakazi wa Kaskazini Mashariki ndio wenye matumaini zaidi kwamba uchumi utaimarika 2021 wakifuatwa na wenzao wa Kati na Nairobi. Lakini wakazi wa Pwani, Magharibi na Nyanza walieleza kukosa matumaini ya mambo kuwa bora mwaka ujao.
Wataalamu wanasema marufuku ya usafiri, sheria ya kutotoka na kuingia baadhi ya kaunti pamoja na amri ya kutotoka nje nyakati za usiku zilikuwa na athari kubwa kwa biashara.
Sekta zote za uchumi ziliathirika, hususan utalii, hoteli na mikahawa, uchukuzi wa umma miongoni mwa sekta zingine, hali iliyopelekea watu wengi kuachwa bila kazi na waliosalia kazini kupunguziwa mishahara.
Kutokana na hali hiyo, Wakenya hawana fedha za kununua chakula, na mahitaji mengine ya kimsingi msimu huu wa Krismasi kwa sababu viwango vyao vya mapato vimepungua pakubwa.
Kulingana na utafiti huo wa Tifa, hizo ndizo sababu zinazosababisha Wakenya wengi kuhisi kuwa hali yao ya kiuchumi ni mbaya zaidi 2020 kuliko ilivyokuwa mnamo 2019.
Hapo jana wakazi wengi wa mijini walikuwa wakiendelea na shughuli zao za kawaida, kinyume na awali ambapo biashara nyingi hufungwa siku chache kabla ya siku ya Krismasi.