Habari Mseto

Krismasi ya dhiki

December 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wanaadhimisha Krismasi ya mwaka huu kwa dhiki kufuatia hali ngumu ya maisha na masharti makali ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Msimu huu ambao kwa kawaida huwa na shamrashara tele, wengi wanalalamika kuwa hawana cha kusherehekea kutokana na matatizo mengi yanayowakumba kibinafsi na taifa kwa jumla.

Hapo jana usiku, Wakristo hawakufika makanisani kama ilivyo kawaida kwa ibada na mikesha ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu, ambayo katika baadhi ya madhehebu huendelea hadi usiku wa manane ama hadi chee.

Hii ni kutokana na kafyu ambayo imekuwa kote nchini na huwa inaanza saa nne za usiku hadi saa kumi alfajiri.Mabaa na maeneo mengine ya burudani na vileo pia yalilazimika kufunga kazi saa tatu za jioni, kinyume na kawaida ambapo usiku wa kuamkia Krismasi wengi hukesha wakiburudika.

Krismasi ya mwaka huu pia inaadhimishwa huku kukiwa na hofu ya maambukizi ya corona kuongezeka, jambo ambalo linazima mbwembwe ambazo wengi wamezoea wakati wa Krismasi hasa kukusanyika kifamilia na katika maeneo ya kustarehe.

Wakenya pia wanakabiliwa na changamoto ya huduma duni za matibabu katika hospitali za umma, na hivyo wananchi ambao kwa bahati mbaya wataugua ama kuhusika kwenye ajali wakati huu watakabiliwa na matatizo ya kupata matibabu.

Kiuchumi, 2020 umekuwa mwaka mgumu kwa Wakenya wengi ambao walipoteza kazi na mapato ya kibiashara kutokana na athari za virusi vya corona, hivyo kuwaacha bila fedha za kusherehekea.Kulingana na Shirika la Takwimu la Kenya (KNBS), watu milioni kumi walipoteza kazi nchini mwaka huu, na wale ambao hawakufutwa walipunguziwa mshahara.

Hali inatarajiwa kuendelea kuwa mbaya hadi 2021 baada ya kampuni nyingi kutoa tahadhari kuwa zitapata hasara, hali inayoashiria kuwa Wakenya zaidi huenda wakapoteza kazi mwaka ujao.KNBS inasema kuwa biashara nyingi zimefungwa na kuacha waliozitegemea bila mapato.

UMASKINI

Shirika hilo linasema hata walio na uwezo wa kifedha watakuwa na ugumu wa kusherehekea Krismasi ya mwaka huu kutokana na masharti ya kuzuia kusambaa kwa corona.

Kulingana na Benki ya Dunia, janga la corona limeongeza kiwango cha umaskini nchini kwa watu milioni mbili.Hata kwa wafanyakazi wa serikali ambao kwa kawaida huwa wanalipwa mapema mwezi Desemba, hali ni tete baada ya Waziri wa Fedha Ukur Yatani kutangaza kwamba serikali haina pesa za kuwalipa mishahara.

Wizara ya Fedha pia haijatoa pesa kwa serikali za kaunti ambazo zingetumia kulipa wafanyakazi na watoaji wa huduma na wauzaji wa bidhaa mbalimbali.

“Hali hii imefanya wengi kukosa pesa za kufurahia Krismasi mwaka huu. Ni bayana kuwa athari za corona zimesukuma Kenya pabaya,” asema mtaalamu wa masuala ya uchumi David Kimotho.

Dhiki ya Wakenya imezidishwa na kurejeshwa kwa viwango vya kodi ambavyo serikali ilikuwa imepunguza kwa miezi saba ili kuwaepusha na athari za corona.

Watalaamu wa uchumi wanasema kurejeshwa kwa viwango hivi wakati Wakenya wanapokabiliwa na hali ngumu ni sawa na kuwadhulumu zaidi.

“Kurejeshwa kwa viwango vya kodi wakati ambao wengi wametumbukia katika umaskini kwa kukosa ajira kunaweza kufanya mambo kuwa mabaya zaidi. Kampuni zilizotumia afueni hiyo kustahimili athari za corona zinaweza kuzama,” mtaalamu wa uchumi Mohamed Wehliye asema.

Huku shule zikitarajiwa kufunguliwa Januari 4, wazazi wanajikuna vichwa kwa kuwa wengi hawana mapato ya kulipa karo na kununua mahitaji muhimu kwa watoto wao.

Shule nyingi zimewapa wazazi masharti makali ya kulipa karo yote ya muhula wa pili kabla ya wanafunzi kuruhusiwa kuanza masomo.Kalenda ya shule imefanyiwa mageuzi na wazazi watahitajika kulipa karo ya mihula minne ndani ya mwaka mmoja, jambo ambalo kwa wengi litakuwa mlima katika mazingira ya sasa ya uchumi.

Lakini dhiki hizo huenda zikapungua kidogo baada ya madaktari kukubaliana na serikali kurejea kazini.Katibu Mkuu wa chama cha Wahudumu wa Afya na Madaktari wa Meno (KMPDU), Dkt Chibanzi Mwachonda jana alisema kuwa walikubaliana na wizara za Leba na ile ya Afya kuhusiana na njia za kutekeleza matakwa yao.

Kwenye taarifa iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Baraza la Magavana, Dkt Mohamed Kuti, serikali na madaktari walikubaliana kuhusu masuala husika.

“Wizara ya Afya itawasiliana na kaunti na idara zote husika serikalini, kuhakikisha masuala ambayo madaktari wameibua yanashughulikiwa,” akasema Dkt Kuti.

Hata hivyo, wagonjwa wataendelea kuhangaika wakati huu wa Krismasi kwa kuwa wauguzi na matabibu wangali katika mgomo.Wahudumu wa afya wamekuwa wakilalamikia kupuuzwa na serikali katika kuwalinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.