• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Korti yaruhusu serikali kujenga nyumba 7,000

Korti yaruhusu serikali kujenga nyumba 7,000

Na SAM KIPLAGAT

SERIKALI sasa iko huru kujenga nyumba 7,000 katika mtaa wa Shauri Moyo, Nairobi, baada ya Mahakama Kuu kufutilia mbali kesi iliyokuwa imewasilishwa na wafanyakazi wake.

Wafanyakazi hao wapatao 330 walifika mahakamani mnamo 2014 ambapo walipata agizo la kuisimamisha Wizara ya Ardhi na Ujenzi dhidi ya kuwaondoa katika nyumba zao ili kutoa nafasi kwa ujenzi huo.

Mradi huo unalenga kuwanufaisha watumishi wa serikali, ambapo watauziwa nyumba hizo kati ya Sh4 milioni Sh25 milioni kwa kipindi cha miaka 20.

Aidha, watatozwa riba ya asilimia tano kila mwaka.

Wawekezaji walikuwa wamepangiwa kujenga nyumba hizo chini ya muungano wa ushirikiano wa serikali na sekta ya kibinafsi (PPP) ambapo wangefadhili ujenzi, wasimamie nyumba hizo kwa muda ili kupata fedha zao kabla ya kurejesha usimamizi wake kwa serikali.

Kwenye mpango huo, serikali ilikuwa imepangiwa kutoa ekari 40 za ardhi katika mitaa mitatu, ili kuwawezesha wawekezaji hao kujenga nyumba hizo za bei ua kadri.

Wafanyakazi walitarajiwa kulipa asilimia 10 ya kiwango cha kwanza, huku fedha zilozobaki wakilipa kwa kiwango kidogo kwa muda wa miaka 20. Hii ilikuwa ni hadi pale wangestaafu kutoka kazi za serikali.

Jumatatu, Jaji John Mativo aliondoa agizo la kusimamisha ujenzi huo. Kwenye uamuzi wake, alisema kwamba hakukuwa na msingo wowote wa kisheria kuizuia kuutekeleza.

Wafanyakazi, walioongozwa na Justus Muthumbi na Timothy Wanyama wanaitaka serikali kuwapa makao mbadala, kabla ya nyumba hizo kubomolewa.

Walisema wamekuwa wakikaa kwa muda mrefu katika nyumba hizo, ambapo wamekuwa wakilipa kodi ya Sh3,000 hadi Sh5,000.

Waliikosoa Wizara ya Ujenzi na Inpekta Jenerali wa Polisi kwa kuwadhulumu na kuwahangaisha kuondoka katika nyumba hizo ilhali bado hawakuwa wamepata makao mbadala.

Walilalama kwamba serikali haijakuwa ikiwashirikisha kwenye taratibu hizo, hivyo wangali gizani ikiwa watapata nyumba mbadala za kuishi na familia zao.

Walisema hawajui ikiwa watatengewa nyumba hizo ujenzi wake utakapokamilika. Kwa hayo, wamesisitiza kwamba lazima haki zao zizingatiwe.

 

 

 

 

 

You can share this post!

Auawa kwa kuchelewesha kulipa deni la Sh100

UFISADI: Wafanyakazi 18 wa Kenya Power wapigwa kalamu

adminleo