Habari Mseto

Daktari aandika wasia akitaka mwili wake utumiwe kwa utafiti akifa

May 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

DAKTARI mmoja kutoka Meru na mmiliki wa zahanati ameandika wasia akiomba mwili wake usizikwe wakati maisha yake yatatamatika humu duniani.

Dkt Cyprian Thiakunu alielezea kuwa familia yake tayari inafahamu matakwa yake, kuwa mwili wake atakapofariki upewe wanafunzi wanaosomea udaktari, hasa upasuaji, akisema kuwa maandalizi ya maziko ni kuharibu pesa, wasaa na rasilimali.

Dkt Thiakunu ambaye aligura kazri yake serikalini mwaka 1992 anasema uamuzi huo ulitokana na ukosefu wa miili ya kufanyia mazoezi y aupasuaji miongoni mwa wanafunzi wa upasuaji kwa kuwa Wakenya wengi huwanyima wanafunzi hao miili ya maabara wakati jamaa wao wanafariki.

Mwanamume huyo, anayemiliki zahanati ya Nyambene, Muringane, kaunti ya Meru, alikumbana na uhaba wa miili ya kufanyia mazoezi ya masomo wakati akiwa katika Chuo Kikuu cha Nairobi kwa miaka 8 hadi 1988. Katika nyakati hizo, miili ya wafu ilikuwa inaagizwa kutoka Uganda.

Wakati wote, daktari huyo amekuwa akitaka kutoa msaada wa mwili wake kwa kuujumuisha katika wasia wake, lakini katiba ya awali haingeruhusu hilo.

Lakini sasa sheria inaruhusu Mkenya yeyote kutoa mwili wake kwa idara za upasuaji vyuoni kwa kuwa kulingana naye “tatizo lililopo Kenya ni kupata miili kwa wanafunzi wa upasuaji, na kwa bahati nzuri Rais Kenyatta ametia saini sheria ya kuruhusu wananchi kupeana miili yao kwa utafiti.”

Alieleza kuwa alinufaika na mwili wa mtu wakati akiwa mwanafunzi na akawaza: “Ninafaa kutoa mwili wangu nikifa ili utumiwe na wanafunzi wengine au watafiti.”