Makala

TAHARIRI: Rais, maafisa wako ndio maadui wakubwa wa maendeleo

May 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

RAIS Uhuru Kenyatta alisema Jumatano kuwa kuna Sh2 bilioni zilizokuwa zimetengwa kwa shughuli ya kuboresha barabara za Nairobi, lakini hafahamu jinsi zilizvyotumika. Matamshi haya yanazua maswali kuhusu kuwajibika kwa wanaotwikwa jukumu la kuhakikisha miradi ya Serikali imetekelezwa kikamilifu.

Ni wazi kwamba maafisa wa Serikali ndio maadui wakubwa wa maendeleo ya nchi, na hata Rais ajaribu jinsi gani kuboresha maisha ya Wakenya, itakuwa vigumu sana maono yake kuafikiwa.

Sasa ni dhahiri kwa Rais Kenyatta kuwa nia yake njema kwa taifa hili imetumiwa na maafisa wake katika ngazi tofauti kutumia vibaya pesa wanazotengewa kutekeleza miradi, huku wakikosa kufanya wanayotakiwa kutekeleza.

Mfano mzuri ni ajenda yake kubwa ya kuboresha NYS ili iwe taasisi kubwa ya kusaidia vijana kupata mafunzo na ujuzi wa kuweza kubuni ajira na kuchangia katika maendeleo ya nchi. Aliweka mabilioni katika taasisi hiyo akitarajia maelfu ya vijana watanufaika. Lakini sasa?.

Rais pia alikuwa na nia njema alipozindua mpango wa kuhakikisha wakulima wameuziwa mbolea kwa bei nafuu. Hii nayo imeshindikana kutokana na watekelezaji kusimamia vibaya na kuruhusu ufisadi. Pia kuna mradi wa Galana ambao mafanikio yake hayajaonekana licha ya mabilioni kuwekezwa huko.

Rais pia asisahau kujitolea kwake katika kusaidia wazee kupata kipato kidogo cha kuwasaidia kimaisha. Badala yake sasa mwanalalamika.

Mifano ni mingi ya miradi ambayo Rais Kenyatta alianzisha akitarajia itasaidia wananchi. Lakini ukweli ni kuwa watekelezaji hawajali nia ya rais na kwao inakuwa ni fursa ya kupora.

Rais anafaa afahamu kuwa maadui wake na taifa kwa jumla ni maafisa ambao anategemea kutekeleza ndoto na maono yake.

Maafisa hawa hawajali na ndiposa utapata wanafanya kazi duni na miradi wanayotekeleza kamwe haina manufaa ya kutajika kwa mwananchi wa kawaida.

Rais anafaa atathmini upya mfumo wake wa utumishi wa umma ili kuhakikisha wale wanaolemaza ndoto zake wamefagiliwa mbali na hawapewi nafasi ya kuvuruga miradi yake.

Ni Gazeti la Kampuni ya Nation Media Group
Mkurugenzi Mkuu: STEPHEN GITAGAMA
Mhariri Mkuu: TOM MSHINDI
Mhariri : PETER NGARE