• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Walimu wachunguzwa kuhusiana na visa vya ubakaji shuleni

Walimu wachunguzwa kuhusiana na visa vya ubakaji shuleni

Na WAANDISHI WETU

WIZARA ya Elimu pamoja na maafisa wa usalama wameanzisha uchunguzi dhidi ya walimu kadhaa wanaokabiliwa na shutuma za kuwanajisi na kuwalawiti wanafunzi katika maeneo mbalimbali nchini.

Jana, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walianza kuchunguza sampuli za DNA za wafanyakazi saba wa kiume wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, Nairobi, wanaoshukiwa kuhusika katika ubakaji wa mwanafunzi wa kidato cha pili. Saba hao wanajumuisha walimu watano, mkufunzi wa michezo ya kuigiza na wafanyakazi wawili wa masuala ya usimamizi wa shule.

Uchunguzi huo umenuiwa kubainisha kama walikuwa mahali hapo mkasa ulipotokea, na pia kama chembe za miili yao ziligusana na za mwathiriwa.Ilidaiwa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 15 alinajisiwa usiku wa kuamkia Jumamosi katika kisa ambapo wanafunzi wengine pia walidai kushambuliwa na watu wasiojulikana.

Waziri wa Elimu Amina Mohamed aliagiza shule hiyo ifungwe uchunguzi unapoendelea.

Jana maandamano yaliandaliwa nje ya shule hiyo ambapo wadau mbalimbali walioshiriki maandamano hayo walitaka mwalimu mkuu asimamishwe kazi ikizingatiwa kuwa miezi michache iliyopita kulikuwa na kisa cha moto kilichosababisha maafa ya wanafunzi 10.

Huku hayo yakijiri, Baraza la Magavana lilitaka serikali ichukulie mkasa huo kwa uzito.

“Ni jukumu la serikali kuhakikishia wanafunzi usalama wao wanapokuwa shuleni,” akasema mwenyekiti wa baraza hilo Josphat Nanok ambaye pia ni Gavana wa Kaunti ya Turkana.

Kwa upande mwingine, wabunge walitaka polisi watumwe kulinda shule zote za wasichana nchini.

Kwenye kikao na wanahabari, wabunge wakiwemo Millie Odhiambo (Suba Kaskazini) na Alfred Keter (Nandi Hills) walitaka serikali itenge fedha zaidi kwa shule ili zijenge kuta.

Ripoti ya Valentine Obara, Stella Cherono, Lucy Mukanyika, Samwel Owino na Nicholas Komu inafaa ichukulie suala la usalama wa wasichana kwa uzito. Hatujui wasichana wetu wangapi wamedhulumiwa na wakakosa kupiga ripoti,” akasema Bi Odhiambo.

Alidai kuwa usiku wa Jumamosi mwanamume aliingia katika bweni la Shule ya Upili ya Wasichana ya Rusinga lakini akapatikana na matroni wa wanafunzi kabla awadhuru.

Kwingineko, polisi wa eneo la Kieni Mashariki, Kaunti ya Nyeri wanamtafuta mwalimu aliyedaiwa kumnajisi msichana wa darasa la nane.

Afisa Mkuu wa polisi katika eneo hilo Job Lesikinwa, alisema uchunguzi wa matibabu ulithibitisha kwamba msichana huyo wa shule iliyo Naromoru alinajisiwa.

Katika Kaunti ya Taita Taveta, maafisa wa elimu wanachunguza mwalimu mkuu wa shule moja ya eneo la Taveta baada ya madai kuzuka kuwa alikuwa akilawiti wanafunzi katika eneo lake la kazi la awali.

Madai hayo yalizuka katika mtandao ambapo mwalimu huyo alishutumiwa kwa kuwalawiti wanafunzi kadhaa huku wengine wakijitokeza na kudai kuwa walikuwa wametendewa tendo hilo la unyama miaka iliyopita.

Afisa wa elimu wa Taveta Bw Abdulatif Hassan alisema kuwa wameanzisha uchunguzi dhidi ya madai hayo.

You can share this post!

Kiini cha Uhuru kusisimka kupiga vita ufisadi

Wakuu wa fedha na ununuzi serikalini watupwa nje

adminleo