DSTV na GOtv kupeperusha Kombe la Dunia kwa Kiswahili
NA PETER MBURU
WATUMIZI wa mitambo ya televisheni ya DSTV na GOtv na wapenzi wa kandanda wana habari njema kwani mwaka huu wataweza kupata matangazo ya Kiswahili kwenye kipute cha Kombe la Dunia.
Aidha, wataweza kujitazamia mechi zote 64 za kombe hilo, ambazo zinatarajiwa kuanza Juni 14.
Tangazo hili limewekwa wazi na maafisa wa kampuni hizo, wakisema wanataka watumizi wa mitambo yao kutoachwa nyuma katika kila hatua ya mechi za kombe la dunia mwaka huu.
Itakuwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kiswahili kutumika katika uchambuzi wa mechi hizo na watumizi watahitajika kuchagua lugha watakayopenda kati ya Kiswahili na kimombo, wakasema maafisa hao.
Kulingana na kampuni ya Multichoice ambayo inafanikisha upeperushaji wa burudani kwa GOtv na DStv, hatua hii inanuiwa kuleta ladha ya Russia, ambapo mechi hizo zitachezewa karibu na Kenya.
Siku za Jumamosi na Jumapili, kampuni hizo pamoja nay a Coca-Cola ziliandaa hafla kubwa mjini Nakuru kama njia ya kuuza wazo la huduma yao mpya kwa wateja, katika kampeni iliyopewa jina ‘Chizika na Russia’.
Maelfu ya vijana pamoja, mashabiki wa kandanda na watumizi wa mitambo hiyo kwa jumla walijitokeza katika hafla hiyo iliyojawa na burudani.
“Tunafurahia kuwapa wateja wetu burudani ya ziada na kuwafanya wajihisi kuwa sehemu ya bidhaa zetu ndipo tukaamua kuja na uchambuzi wa Kiswahili jambo ambalo halijafanyika mbeleni ili kuwaridhisha,” akasema meneja mkuu wa GOtv Kenya, Bw Simon Kariithi.
Mechi zote 64 zitatazamwa na watumizi wa mitambo ya GOtv na DStv kupitia mifuko ya Access, Family, Compact na Compact Plus
Bw Kariithi aliongeza kuwa kutakuwa na mtambo teule wa Superspot ambao utawaelimisha watazamaji kuhusu historia ya kombe la dunia.
“Tunataka kuwaweka watazamaji wetu makini kila wakati kuhusu maswala ya kandanda katika kipindi hicho cha mwezi mmoja. Wakati hawatazami mechi, tutawaelimisha kuhusu maswala anuwai ya kandanda,” akasema Meneja huyo.
Kulingana na kampuni hizo, tangazo hilo limeibua uchangamfu miongoni mwa watumizi wa bidhaa zao, huku likiinua soko lao.