Wanyama hawa wanaofanya ngono saa 14 mfululizo wako hatarini
MASHIRIKA na VALENTINE OBARA
QUEENSLAND, AUSTRALIA
WATAFITI wanajitahidi kupata jinsi watakavyozuia aina ya wanyama wafanyao ngono kwa zaidi ya saa 14, wasiangamie kutoka ulimwenguni.
Wanyama hao wanaofahamika kama ‘marsupials’ (pichani) wameingizwa kwenye orodha ya wanyama ambao wamo hatarini kutokomea ulimwenguni.
Hii ni kutokana na kuwa madume huwa na mazoea ya kufanya ngono kwa saa 14 mfululizo, hali inayowachosha na kufanya wafe punde baadaye.
Kulingana na ripoti, watafiti wa Chuo Kikuu cha Queensland kilicho Australia wameamua kuanzisha utafiti ili kuokoa wanyama hao waliogunduliwa mwaka wa 2013.
Mtaalamu wa masuala ya wanyama katika chuo hicho, Dkt Anrew Baker, alinukuliwa kusema kuwa afya ya wanyama hao hudhoofika kwa kasi baada ya kupandiana kwa saa nyingi mfululizo.
Ilisemekana dume huruka kutoka kwa jike mmoja hadi mwingine bila kupumzika hasa mwishoni mwa msimu wa majira ya baridi.
“Nimewahi kuwaona wakitembea mchana baada ya kufanya ngono usiku mzima, bado wakiwa wanatafuta majike ya kupandia, huku wakivuja damu kwenye sehemu nyingi za miili yao na manyoya yameng’oka,” akasema.
Ripoti zinasema jike huweza kuishi kwa miaka miwili na kupata watoto kati ya sita na 14, huku madume wakifariki hata kabla kukamilisha mwaka mmoja.