• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Wazazi kupokea maiti ya mwanao aliyewapuuza 1980

Wazazi kupokea maiti ya mwanao aliyewapuuza 1980

Na LUCY MKANYIKA

FAMILIA moja katika eneo la Ngerenyi, Kaunti ya Taita Taveta sasa ina matumaini ya kumzika mwana wao aliyefariki ng’ambo miezi mitatu iliyopita. 

Marehemu Justin Kitogho alifariki Marekani mnamo Machi 11, 2018 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Wakenya wanaoishi Marekani ndio waliochanga fedha za kusafirisha mwili na kugharamia mazishi.

Marehemu alihamia Marekani mnamo 1980 baada ya kupata udhamini wa masomo ya sayansi.

Kulingana na mamake, Bi Evence Mwashighadi (pichani kulia), mwanawe alikata mawasiliano mara alipoondoka Kenya na hakuwahi watumia hata senti moja.

“Mwanangu alipotelea ng’ambo. Tangu nipate habari za kifo chake nimekuwa na uchungu moyoni kwani sikuwa na uwezo wa kuuleta mwili wake nyumbani,” akasema Bi Mwashighadi.

Alieleza Taifa Leo kuwa ingawa mwanawe huyo alitelekeza familia yake, alikuwa amemsamehe.

“Tangu aende hajawahi kunitumia chochote. Sijui alikuwa yuaishi wapi wala na nani,” akasema ajuza huyo.

Alisema kuwa amekuwa akiishi maisha ya umaskini na mara kwa mara akikosa fedha za kuwalea wajukuu ambao wanamtegemea.

“Nyumba yangu ni duni, sina chakula na mavazi. Lakini la muhimu zaidi ni nione mwili wa mwanangu,” akasema.

Mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa hadi nchini Kenya na kisha kuzikwa mnamo Jumamosi hii.

Mwakilishi wadi ya Wusi/Kishamba, Bw Justin Juma alisema kuwa wenyeji wa kijiji cha Ngerenyi wanashughulika kupokea mwili huo tayari kwa mazishi.

Hata hivyo wanakijiji hao wamekosa kutoa usaidizi kabla ya familia hiyo kutoa takriban sh4500 kama faini ya marehemu kutohusika katika hafla za mazishi eneo hilo.

“Kuna sheria kuwa ikiwa mtu hajihusishi na shughuli za kijiji, wakati yeye anapatwa na matatizo lazima atoe faini ya Sh4500,” akasema mwenyekiti wa kijiji cha Ngerenyi, Bw Mwadime Kitogho.

“Hata kama hatumjui ni vyema azikwe kwa heshima kwani ni ndugu yetu. Pia tukumbuke kuwa hatufai kusahau jamii zetu tunapofanikiwa kimaisha,” akasema Bw Juma.

You can share this post!

Kundi la kwanza la madaktari wa Cuba latua nchini

Wakenya wengi hawana habari wanaugua Ukimwi – Wizara...

adminleo