HabariSiasa

SAKATA YA NYS: Washukiwa kusalia ndani hadi Juni 12

June 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

KIZINGITI kikuu kilikumba kesi dhidi ya washukiwa 46 wa sakata ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) walipopinga ikiendelea kabla ya kupewa nakala za mashahidi 36.

Mawakili 35 wanaowatetea washukiwa hao walizua tetezi kali wakisema “kuna msukumo kesi hiyo iamuliwe kwa upesi kuridhisha umma kwamba vita dhidi ya ufisadi vimepamba moto.”

Mawakili hao waliomba kesi hiyo iahirishwe kwa muda wa wiki mbili wapokee nakala za mashahidi katika kesi ya ulaghai wa Sh59 milioni za NYS.

Kufuatia ombi hilo hakimu mkuu mahakama ya kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 12 atakapoamua kuhusu nakala za mashahidi zinazodaiwa.

Mawakili Kirarhe Wandugi (kushoto ), Dunstan Omari (kati) na Cliff Ombeta wapinga kesi dhidi ya washukiwa wa sakata ya NYS ikianza wakisema hawajapewa nakala za ushahidi. Picha/ Richard Munguti

 Pia alimwagiza Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) awakabidhi mawakili ushahidi uliopo ifikapo Juni 13 kisha akatenga Juni 20 siku ya mawakili kueleza muda watakaochukua kuwahoji mashahidi kesi hiyo ya ulaghai wa Sh59milioni dhidi ya  Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai, Katibu MkuuWizara ya Masuala ya Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia  Bi Lillian Omollo na washukiwa wengine wanaodaiwa walimlipa Bi Ann Wambere Ngirita zaidi ya Sh59milioni kwa huduma ambazo hakutoa kwa shirika hilo la Serikali.

Bw Ogoti alifahamishwa haki za washukiwa zimo hatarini kwa vile DPP amekaidi agizo la awape washukiwa nakala za mashahidi.

“Kesi hii haipasi kuendelea hata nukta moja ikiwa washukiwa hawana nakala za mashahidi. Katiba imeweka wazi utaratibu wa kufuatwa,” alisema wakili Cliff Ombeta

DPP kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Bi Emily Kamau alisema hajakataa kuwapa washukiwa ushahidi.

Mchoro huu katika mkono wa kushoto wa Bi Anne Ngirita ulizua msisimko katika mitandao ya kijamii. Picha/ Richard Munguti

Bw Ogoti alifahamishwa matamshi yake kuwa zaidi ya Sh9 bilioni zilitoweka na habari zinazochapishwa na vyombo vya habari kuhusu sakata hii ni wazi haraka ipo ya kuwasukuma jela washukiwa.

Bw Ombeta alisema matamshi ya Jaji Mkuu David Maraga kuhusu majaji na mahakimu wanaosikiza na kuamua kesi za ufisadi yamaanisha “ wahusika wapasa kusukumwa jela upesi.”

Bw Ndubai na washukiwa wengine 21 walishtakiwa Mei 29 na washukiwa wengine 20 kushtakiwa Juni 4, 2018.

Wengine watatu Josephat Njoroge, Anthony Wamiti na Peter Kimani ambao ni wakurugenzi wa Arkroad Supplies Limited iliyolipwa Sh24 milioni walishtakiwa baada ya kujisalamisha kortini Jumanne.