Shule ya Moi Girls yafunguliwa
Na WANDERI KAMAU
WANAFUNZI katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, Nairobi, walirejea shuleni jana baada shule hiyo kufungwa kwa wiki moja kutokana na kisa cha ubakaji wiki iliyopita.
Wanafunzi walitakiwa kufika shuleni humo kufikia saa nane, ambapo walisajiliwa katika lango kuu.
Aidha, waliandamana na wazazi wao. Baada ya kusajiliwa, wazazi waliruhusiwa kuzuru mabweni hadi mwendo wa saa tisa alasiri.
Leo, maafisa kutoka Wizara ya Elimu na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) watafanya mkutano wa pamoja na wazazi hao kuhusu hali ilivyo shuleni humo.
Vilevile, wanafunzi watapewa ushauri maalum kufuatia kisa hicho.
Kulingana na ratiba iliyotolewa na wizara, masomo yamepangiwa kuanza rasmi kesho.
Mnamo Jumamosi, Waziri wa Elimu Amina Mohamed aliteua bodi ya muda ya watu tisa kuendesha shughuli za usimamizi wa shule hiyo.
Kundi hilo linaongozwa na Mshirikishi Mkuu wa Masuala ya Elimu katika Kaunti ya Nairobi John Ololtuaa ili kuchukua mahali pa bodi ya zamani, ambayo ilivunjwa na waziri. Bodi hiyo mpya ina wawakilishi kutoka TSC na Wizara ya Elimu.
Wanachama wengine wanajumuisha Bi Rose Ombeva, Bi Lydia Mutegi, Bw Bernard Kimachas, Bw Gichuhi Ndegwa, Bw Rashid Mohamed na Bi Fidhelis Nakhulo kutoka makao makuu ya wizara.
Wawakilishi wengine kutoka TSC ni Bi Lucy Mugambi na Cicely Musyoki.
Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi Florence Omusula ndiye kaimu katibu wa bodi hiyo.
Tayari, Bi Mohamed ashabuni kundi maalum kubuni mikakati ambayo itatumika kukabili dhuluma za kimapenzi shuleni humo.