• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Niachie ugavana uingie mbio za Ikulu, Wavinya amwambia Mutua

Niachie ugavana uingie mbio za Ikulu, Wavinya amwambia Mutua

Na STEPHEN MUTHINI

ALIYEKUWA mgombeaji wa kiti cha ugavana Kaunti ya Machakos, Bi Wavinya Ndeti amemtaka Gavana Alfred Mutua aendeleze kampeni za urais na kumuachia kiti cha ugavana ili awahudumie wakazi wa kaunti hiyo.

Bi Ndeti alisema kwa sababu Bw Mutua ameanza kutembea kote nchini akijipigia debe kuchaguliwa rais 2022, inamaanisha ameacha kuhudumia watu wa Kaunti ya Machakos.

Akiongea katika kanisa Katoliki la Katheka wadi ya Vyulya Jumapili, Bi Ndeti alisema hana mipango ya kugombea urais na atatumia nguvu zake kuletea watu wa Machakos Maendeleo.

“Sitaki kugombea urais. Ninataka kuwa gavana wa Machakos. Ninamuuliza Mutua aniachie kiti cha ugavana na aendelee kugombea urais,” alisema Bi Ndeti.

Aliwaomba wapigakura wanawake kutodanganywa kwamba mwanamke hawezi kuongoza akitaja Gavana wa Kaunti ya Kitui Charity Ngilu ambaye ameongoza kaunti yake vyema.

Wakati huo chama cha wafanyabiashara tawi la Machakos kimewataka wafanyabiashara kutolipa kodi kwa serikali ya Gavana Mutua kikidai anatumia vibaya pesa zao.

“Tunapomuona Mutua akitembelea Nyeri na Nyamira tunajiuliza iwapo anatumia kodi yetu kwa kampeni zake za urais. Tunaumwa sana,” alisema mwenyekiti wa tawi hili Bw Simon Kitheka.

Alisema alipata agizo la mahakama kusimamisha wenye mahoteli na baa kulipa kodi.

Hata hivyo, washirika wa Bw Mutua akiwemo aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Bw Kalembe Ndile walisema uamuzi wa mahakama wa kubatilisha ushindi wake ulikuwa wa kisiasa.

“Tunaona mkono uliofichika kwenye uamuzi huo. Tulimuona Gavana Mutua akisalimiana na Gideon Moi na tunajua baadhi ya watu hawakufurahia,” alisema Bw Ndile na kuongeza kuwa siasa za urithi za 2022 zinachezwa kortini.

Alimtaka Jaji Mkuu David Maraga kuchunguza kinachotendeka mahakamani.

Bw Ndile alimwambia Gavana Mutua kutokuwa na wasiwasi kwa sababu ana wafuasi wengi na atakabiliana na uamuzi huo kisiasa.

You can share this post!

Mawakili wataka Uhuru na Ruto watangaze mali yao

RAMADHANI: Chunguza saum yako ukiwa katika ndoa ya aina hii

adminleo