• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
TAHARIRI: Serikali ijitolee kuzima gonjwa

TAHARIRI: Serikali ijitolee kuzima gonjwa

Na MHARIRI

MLIPUKO wa kipindupindu unaendelea kuenea maeneo mbalimbali nchini na kuna haja ya hatua za haraka kuchukuliwa ili kuepuka maambukizi na vifo zaidi.

Inatishia zaidi kuona maradhi hayo yameenea hadi jiji kuu Nairobi kutokana na mfumo mbaya wa kusambaza maji safi ya kutumia.

Siku chache zilizopita, watu 78 eneo la Madogo Kaunti ya Tana River waliambukizwa maradhi hayo wengi wao wakiwa watoto na kina mama.

Mwishoni mwa mwezi uliopita Shirika la Afya Duniani (WHO), liliionya Kenya kuhusu kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini na kwamba ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa, basi kuna uwezekano ugonjwa huo ukaenea taifa lote.

WHO ilionya kuwa kukosekana kwa majisafi na salama ya kunywa ndiyo sababu kuu ya kuenea kwa kasi kwa kipindupindu Kenya, hivyo kuna haja ya serikali kuchukua hatua za haraka kusafisha maji yanayotumiwa na raia.

Hatutaki kusambaa kwa kipindupindu kufikie viwango vya serikali kuhitajika kutangaza ugonjwa wa kipindupindu kuwa janga la taifa, badala yake taasisi husika zinapaswa kuweka juhudi za haraka kuutokomeza ugonjwa huu ambao unalitia aibu taifa letu.

Kuendelea kuenea kwa ugonjwa huu ni aibu ya taifa letu kwa sababu chanzo cha kuenea kwa ugonjwa huu kinajulikana, kwamba ni kula chakula au maji yenye vimelea vya “Vibrio cholera” ambavyo ndivyo husababisha ugonjwa wa kipindupindu.

Vimelea hivi hupatikana kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au kwenye kitu chochote kilichochafuliwa na kinyesi au matapishi ya mgonjwa.

Rai yetu kubwa ni kwamba serikali na wananchi wanatakiwa kuonyesha dhamira ya kweli ya kupambana na ugonjwa huu, kwanza kwa kuhakikisha kunakuwa na miundombinu bora ya majitaka, kutupa uchafu katika sehemu sahihi, kuwepo maji safi ya kunywa, kuchemsha maji ya kunywa pamoja na watu kujifunza utamaduni wa kunawa mikono kwa sabuni kila wanapotoka chooni.

Tunaamini pia serikali za kaunti zitalichukulia suala la ugonjwa wa kipindupindu kuwa moja ya vipaumbele vyake, kwa kutoa maafisa na raslimali zaidi kuboresha afya ya Wakenya mashinani.

Tunachotaka ni kuona viongozi pamoja na maafisa wa afya wakipita mitaani na kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kupambana na ugonjwa huu.

Ni Gazeti la Kampuni ya Nation Media Group
Mkurugenzi Mkuu: STEPHEN GITAGAMA
Mhariri Mkuu: TOM MSHINDI
Mhariri : PETER NGARE

You can share this post!

Hofu ya ulevi wa jombi yafikisha mke kwa bosi

Watupa mtoto kwa kukejeliwa kuzaa watoto wengi

adminleo