Jela miezi 6 kwa kupanda bangi kanisani akidai ni maua
Na TITUS OMINDE
MWANAUME mmoja alifungwa jela Jumatatu na mahakama ya Eldoret baada ya kupatikana na hatia ya kupanda mmea wa bangi katika shamba la watawa dayosisi ya kanisa la Katoliki mjini Eldoret.
Mahakama iliambiwa kuwa Joash Kiplimo Chirchir ambaye hufanya kazi katika shamba hilo liloko katika mtaa wa Kimumu mjini Eldoret, alipatikana akiwa amepanda mashina 1,000 ya mmea huo shambani humo mnamo Juni 3.
Watawa husika hawakuwa wanajua mmea kwani waliugundua baada ya kuita majirani kuwasaidia kuutambua.
Majirani waliwaelezea kuwa mmea huo ulikuwa ni bangi ambapo ni hatia kuupanda.
Watawa hao waliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Kapsoya ambapo polisi walifika shambani humo na kushika mshukiwa kabla ya kung’oa mmea huo.
Mshtakiwa alikiri mashtaka dhidi yake mbele ya hakimu mkuu wa Eldoret.
Wakati wa kujitea mshtakiwa alisababisha kicheko mahakamani alipoambia mahakama kuwa hakuwa na nia mbaya kupanda mmea huo bali aliupanda kama maua huku akitaka mahakama imsamehe.
Akitoa hukumu yake hakimu alisema kifungo cha juu cha makosa kama hayo ni kufungwa jela kwa miaka mitano au faini ya Sh250,000 hata hivyo, alimuonea mshtakiwa huruma na kumfunga kwa miezi sita au kutozwa faini ya Sh50,000.
Wiki jana katika mahakama hiyohiyo, watu wengine wanne walikiri mashtaka ya kupatikana na misokoto zaidi ya 200 ya bangi.
Idadi kubwa ya washtakiwa hao walikuwa vijana ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa shule moja ya upili katika kaunti ya Uasin Gishu.
Washtakiwa hao ambao walinaswa katika mitaa mbalimbali mjini Eldoret wanatarijiwa kuhukumiwa wiki hii.