Makala

RAMADHANI: Ni lazima maskini pia wapewe cha kusherehekea Idd

June 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na KHAMIS MOHAMED

ALHAMISI majaaliwa Waislamu kote ulimwenguni wataelekeza macho mbinguni ili kuutafuta mwezi wa kukamilika kwa Ramadhani. Kalenda ya Kiislamu hutegemea kuandama kwa mwezi na huwa na siku 29 au 30.

Alhamisi ni siku ya 29 na kwa hivyo, watu watatazama kwa makini kuona kama watakuwa wanatamatisha ibada ya kufunga au watakamilisha siku 30 Ijumaa na kusherehekea Idd Jumamosi.

Idd-ul-fitri ni siku muhimu sana kwa Waislamu, kwa kuwa huwa wanaadhimisha kumaliza salama kipindi cha ibada ya kujinyima yote mazuri ambayo wako nayo.

Kutokana na umuhimu wa siku kama hii, Uislamu unamlazimu kila aliyefunga au hata Mwislamu ambaye kutokana na sababu za kueleweka, hakufunga, awalishe masikini siku ya Idd.

Ulishaji huu huitwa Zakaatul-Fitri. Mbali na kuhkikisha kuwa hata wenye shida katika siku hiyo wanasherehekea, pia hutolewa ili kuziba makosa yanayoweza kuwa yamemtokea mtu katika swaumu yake.

Mtume Muhammad (S.A.W), alifanya kutoa Zakaatul-Fitri kuwa lazima, ili kumtahadharisha mfungaji kutokana na maneno na matendo machafu.

Na ili iwe chakula kwa masikini, atakayeitoa kabla ya swala basi hiyo ndiyo zaka yenye kukubaliwa. Na atakayeitoa baada ya swala, basi hiyo ni sadaka kama sadaka nyinginezo.

Zakaatul-Fitri ni wajibu kwa kila Mwislamu, mwenye kumiliki chakula chake na familia yake cha siku ya Idd, kinachozidi hapo ni wajibu akitoe kwa wengine.

Wanaopaswa kupewa Zakaatul-Fitri ni maskini, watumwa (mateka), waliolemewa na madeni, wasafiri waliokwama miongoni mwa wengine.

Mzee wa boma anapaswa kutoa kilo mbili na nusu za chakula kinachopendwa katika eneo alipo, kwa niaba yake na kilo kama hizo kwa kila jamaa wa familia yake anayemtegemea. Hawa ni pamoja na mke, watoto, mayatima anaowalea, na wazazi wawili kama ni wakongwe na wanamtegemea yeye.

Abdillah Ibn Tha’alabah (R.A) amesema kuwa “Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alihutubia siku moja au mbili kabla ya Eid. Akasema “Toeni kibaba cha ngano, au kibaba cha tende au cha shayiri. (Mtoleeni) kila muungwana au mtumwa, mkubwa au mtoto.” Abuu Daawoud.

Wakati bora kabisa wa kutoa Zakaatul-Fitri ni ule usiku wa kuamkia siku ya Idd. Na ni wajibu itolewe kabla ya kuswaliwa swala ya Idd.

Na wajibu wa kutoa hauondoki kwa sababu ya kuchelewa kutoa. Bali itakuwa ni deni linlomsubiri yule abaye kwa mujibu wa sheria zaUislamu, alipswakutoa. Itamlazimu kulipa deni hilo hata mwishoni mwa umri wake, kwa sababu aliwajibikiwa na akafanya uzembe kutoa.

Kwahivyo ndugu msomaji ambaye ulijitolea mwezi mzima kufunga, usifanye saum yako ikose kufika kwa Mwenyezi Mungu ikiwa safi, kwa kupuuza kutekeleza amri hii muhimu.