Habari Mseto

Al Shabaab waua polisi 8 kwa bomu Wajir

June 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

POLISI wanane walifariki Jumapili wakati gari walimokuwa wakisafiria lilipokanyaga bomu katika eneo la Bojigaras, Kaunti ya Wajir.

Wakuu wa polisi walithibitisha kisa hicho huku walioshuhudia wakisema gari liliharibiwa vibaya na waathiriwa walifariki papo hapo.

Mshirikishi wa serikali katika eneo la Kaskazini Mashariki, Bw Muhammad Saleh, alisema waliotega bomu hilo walitoroka mara moja baada ya mlipuko kutokea.

Kulingana naye, uchunguzi wa mapema umeonyesha waliohusika ni washirika wa kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Kikosi cha polisi kilitumwa eneo la mkasa lakini hakuna mwathiriwa yeyote aliyeokolewa.

Shambulio hilo lilitokea wakati ambapo kumekuwa na ilani nyingi kutoka kwa idara ya polisi kitaifa kuhusu uwezekano wa mashambulio ya kigaidi nchini.

Mnamo Juni 6, maafisa sita wa polisi waliuawa na wengine watatu wakajeruhiwa wakati gari lao lilipokanyaga bomu katika eneo la Liboi, Kaunti ya Garissa.

Eneo la mkasa lililo Harhar liko chini ya kilomita mbili kutoka mpaka wa Kenya na Somalia.

Maafisa hao wa kikosi cha GSU walikuwa wakipiga doria wakati mkasa ulipotokea, na walikuwa wametoka katika kambi ya GSU iliyo Harhar.

Ripoti zingine ambazo hazingeweza kuthibitishwa zilisema walikuwa wakifanya msako wa sukari haramu wakati walipokumbwa na kisa hicho.

Wakazi walikuwa wamepiga ripoti kwa polisi kuhusu mienendo ya watu walioshukiwa kuwa magaidi wanaopanga kutekeleza mashambulio.

Magaidi wa Al Shabaab wamekuwa wakilenga maafisa wa usalama katika maeneo ya mpakani kwa kulipua magari yao kwa mabomu ya kutegwa ardhini.

Magaidi hao wanalenga Kenya kutokana na hatua yake ya kuwapeleka wanajeshi nchini humo kuwakabili na kusaidia serikali ya nchi hiyo.