TANZIA: Seneta Ben Okello aliyekuwa mtangazaji maarufu afariki
Na CECIL ODONGO
SENETA wa Migori Ben Oluoch Okello Jumanne alifariki katika hospitali ya MP Shah mjini Nairobi alikokuwa amelazwa kupokea matibabu baada ya kuugua ugonjwa wa saratani ya koo kwa muda mrefu.
Kulingana na mpwa wake ambaye pia ni msemaji wa familia Mark Okundi, seneta huyo aliaga dunia dakika chache baada ya saa sita usiku wa kuamkia jana.
“Aliaga dunia dakika chache baada ya saa sita usiku na amekuwa akiugua kwa muda mrefu saratani ya koo,” akasema Bw Okundi.
Taarifa kuhusu kufariki kwa marehemu pia ilidhibitishwa na mkurugenzi wa mawasiliano katika ofisi yake ya kaunti, Oguda Walter.
“Tunasikitika kuwaeleza wananchi kwamba seneta wetu ameaga dunia. Tuiombee familia yake wakati huu mgumu wa maombolezi,” akasema Bw Oguda.
Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alikuwa miongonio mwa viongozi wakuu kutuma risala zao za rambirambi kufuatia kifo cha seneta huyo.
Bw Odinga ambaye chama chake kilimpoteza seneta wake alimtaja marehemu kama aliyekuwa mkakamavu na mpole licha ya kuigua ugonjwa huo kwa muda mrefu.
“Ben alikuwa mtu jasiri hata kama alikuwa akiugua. Alikuwa mtu mwenye maono aliyewajali waliomchangua. Chama cha ODM kimempoteza mwanachama ambaye bado hakuwa ametekeleza malengo yake kwa raia,” akasema Bw Odinga kwenye risala yake ya rambirambi.
Kwa upande wake Gavana wa Migori Okoth Obado alisema alipokea habari za kifo cha mwendazake kwa mshtuko mkubwa na akamtaja kama mtu aliyekuwa mstari wa mbele kupigania umoja wa viongozi wa kaunti hiyo.
“Kifo kimetupokonya mwanahalisi wa Migori ambaye alipenda amani na uongozi wa kushirikiana. Kwa niaba ya familia yangu na watu wa kaunti hii natuma rambirambi zangu kwa familia ya Ben,” akasema Bw Obado.
Viongozi wengine waliotuma risala zao ni Afisa mkuu mtendaji wa NASA Norman Magaya, Mbunge wa Uriri Mark Nyamita, Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo, Babu Owino wa Embakasi Mashariki, mwakilishi wa kike wa kaunti ya Homabay Gladys Wanga, aliyekuwa mbunge wa Rongo Dalmas Otieno wazee wa jamii ya waluo na viongozi wengine.
Marehemu Ben Oluoch Okello alikuwa mwanahabari msifika kabla ya kujitosa kwenye ulingo wa kisiasa mwaka jana. Alihudumu kama mtangazaji katika shirika la habari la KBC kisha akajiunga na Kampuni ya habari ya Royal Media Services.
Alikuwa mtangazaji wa idhaa ya lugha ya mama ya Ramogi FM ambapo aliandaa kipindi cha kila asubuhi cha ‘Kogwen’ kilichoshabikiwa na jamii ya waluo kwa kuwa kiliangazia maswala mengi ya kijamii.
Katika uchaguzi wa Agosti mwaka jana umaarufu wake kama mtangazaji ulimsaidia pakubwa kushinda kiti cha useneta na kumrithi aliyekuwa seneta Wilfred Machage ambaye hukutetea kiti chake ila akawania ubunge wa Kuria Magharibi.
Marehemu Ben Oluoch Okello aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 55 na amewaacha nyuma mjane na watoto.