• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Sukari ya magendo sasa yanaswa Lamu

Sukari ya magendo sasa yanaswa Lamu

NA KALUME KAZUNGU

POLISI katika Kaunti ya Lamu wamenasa magunia zaidi ya 80 ya sukari ya magendo yenye thamani ya Sh402,500.

Magunia hayo yalinaswa kwenye msako mkali uliotekelezwa Jumatano jioni na mapema Alhamisi asubuhi kwenye miji ya Lamu, Mpeketoni na Kiunga mpakani mwa Lamu na Somalia.

Akithibitisha ripoti hiyo Alhamisi, Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi, alisema washukiwa watano walikamatwa wakati wa msako huo.

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi (kulia) akishirikiana na OCS wa Lamu Magharibi, Paul Mbithi kuinua gunia la sukari ya magendo iliyonaswa na kufikishwa kituo cha polisi cha Lamu Magharibi Alhamisi, Juni 21, 2018. Picha/ Kalume Kazungu

Alisema pia walifaulu kunasa mashini zinazotumika kwenye mchezo wa kamari ilhali washukiwa wengine watatu wakitiwa mbaroni mjini Hindi kwa kuhusika na uendelezaji wa mchezo huo wa kamari.

Bw Kioi alisema operesheni kali ya kusaka bidhaa za magendo inaendelezwa kwenye miji yote ya Lamu na hata vijijini na akaonya kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayepatikana akijihusisha na uingizaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa za magendo hasa sukari eneo hilo.

Alisema tayari wameongeza doria za polisi barabarani na baharini na akaamuru kwamba magari na boti zote za kubeba mizigo vipekuliwe kwanza kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari.

“Tumenasa magunia zaidi ya 80 ya sukari ya magendo ambayo thamani yake ni Sh 402,500. Tumekamata washukiwa watano. Pia tumenasa mashini za kuchezea kamari na kuwashika wahusika watatu wa mchezo huo.

Polisi wakionyesha baadhi ya magunia ya sukari bandia iliyonaswa Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Wote watafikishwa kortini wakati wowote kuanzia sasa. Tunafahamu kwamba sukari ya magendo tuliyoipata Lamu imetoka Mombasa. Kuanzia sasa lori zote zinazobeba mizigo na kutumia barabara ya Lamu hadi Garsen zitapekuliwa na polisi kwanza kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari zao. Pia boti zitapekuliwa baharini. Msimamo wetu ni kwamba tukomeshe kabisa sukari ya magendo kuingizwa hapa Lamu,” akasema Bw Kioi.

Aliwaonya wenye maduka ya jumla na vioski kuepuka kununua na kuuzia wateja wao bidhaa za magendo.

Pia aliwataka wakazi kupiga ripoti kwa polisi iwapo watapata bidhaa wanazoshuku kuwa ghushi zikiuzwa Lamu.

“Msako wetu si wa sukari tu. Tutakagua na kukamata bidhaa zote haramu. Yumearifiwa kuna maziwa bandia yanauzwa Kiunga na maafisa wetu wako huko kuchunguza na kunasa bidhaa hizo. Wananchi tushirikiane ili kuangamiza bidhaa ghushi ambazo zinahatarisha maisha yetu,” akasema Bw Kioi.

You can share this post!

Mchunguzi wa Uswizi atoboa siri ya Anglo-Leasing

Wakurugenzi wanaopokea mshahara mara 50 ya wafanyakazi

adminleo