Jela miaka 3 kwa kulisha umma nyama ya paka kwa miaka 6
JOSEPH OPENDA na MERCY KOSKEY
MAHAKAMA ya Nakuru Jumatatu ilimfunga mwanamume miaka mitatu gerezani kwa kuuzia wauzaji wa sambusa nyama ya paka.
Hakimu Mkuu Benard Mararo alimpata Bw James Mukangu Kimani na hatia alipokiri kosa hilo wakati alipofikishwa mahakamani.
Bw Kimani alishtakiwa kwa kuchinja na kuuza nyama ya paka kwa wateja ambao hawakufahamu, kosa lililotendwa mnamo Juni 24 mjini Nakuru.
Hati ya mashtaka ilisema aliwachinja paka kwa minajili ya kuliwa na binadamu kwa njia ya ulaghai na kukiuka sheria zinazosimamia masuala ya vyakula, dawa na kemikali.
Alikabiliwa pia na shtaka la kuchinja mnyama katika eneo lisilostahili, kinyume na sheria za kudhibiti biashara ya nyama nchini.
Mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka miwili gerezani au faini ya Sh200,000 kwa kosa la kuchinja paka kwa minajili ya kuliwa na binadamu, na mwaka mmoja au faini ya Sh50,000 kwa kosa la pili la kuchinja mnyama katika eneo lisilostahili kisheria. Atatumikia adhabu hizo gerezani mfululizo.
Bw Kimani alikamatwa baada ya kupatikana akimchuna ngozi paka mnamo Juni 24 katika eneo la Showground mjini Nakuru.
Awali alikiri kwamba aliuza zaidi ya paka 1,000 kwa wachuuzi wa sambusa na hoteli za mjini humo tangu mwaka wa 2012.
Mshukiwa huyo alisema alianzisha biashara hiyo alipotambua kuwa kulikuwa na “mahitaji katika soko”.
Alifichua pia kwamba ana soko la ngozi ya paka na yeye hupata kiasi cha pesa kisichopungua Sh500 kwa kila paka anayemchinja.
Hata hivyo, alijitetea kwamba alikuwa ametumwa na mtu ambaye aliahidi kumlipa vizuri iwapo angeuza nyama hiyo na ngozi.
Lakini mahakama ilishikilia msimamo kwamba hukumu aliyopewa ilikuwa sambamba na kosa alilofanya. Mzoga wa paka ulioletwa mahakamani kama ushahidi, baadaye ulichukuliwa na maafisa wa afya ya umma kutupwa kwa njia salama.