Moi taabani kukosa kuhudhuria hafla ya kanisa
FLORAH KOECH na WYCLIFFE KIPSANG
MAZOEA ya Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi kuhudhuria karibu hafla zote za umma kwa helikopta, yamemweka taabani pa wafuasi wake baada ya kukosa kuhudhuria hafla ya kanisa kutokana na hali mbaya ya hewa.
Mwenyekiti huyo wa Chama cha KANU, alistahili kuwa mgeni mkuu Jumapili katika ufunguzi rasmi wa kanisa la Kipsaraman Full Gospel Churches of Kenya lililo Kaunti Ndogo ya Baringo Kaskazini.
Waumini wa kanisa hilo na wafuasi wa chama chake walivunjwa moyo baada ya msaidizi wake kuwasilisha ujumbe kwamba seneta huyo hangefika.
Baadhi ya wafuasi wa chama walikuwa wamesafiri kutoka maeneo ya Nakuru, Nandi na Bomet. Walisikika wakimkosoa seneta huyo waziwazi na kusema hachukulii kwa uzito azimio lake la kuwania urais 2022 na mienendo yake inampiga jeki Naibu Rais William Ruto.
Walimkashifu kwa kutojali maslahi ya wananchi wa kawaida na kutosafiri kwa barabara na badala yake kutumia ndege jinsi afanyavyo anapohudhuria hafla nyingi na ana sifa ya kuita helikopta anayotumia ‘baiskeli’.
“Huyu ndiye mtu anayetuambia kwamba atamshinda Ruto mwaka wa 2022? Kama hawezi kusafiri kwa barabara hata siku moja, atawezaje kushindana na mtu ambaye anaweza kufanya hata mikutano kumi ya hadhara kwa siku moja?” afisa wa kanisa akashangaa.
Jumapili, naibu rais alizuru Kaunti ya Narok ambapo alihudhuria ibada ya pamoja ya makanisa tofauti katika Shule ya Upili ya Sogoo.
Bw Ruto na seneta huyo wamekuwa mahasimu wa kisiasa huku kila mmoja wao akijitahidi kudhibiti siasa za Rift Valley, na wote wanamezea mate urais mwaka 2022.
Kufikia sasa, naibu rais amezuru ngome ya kisiasa ya Bw Moi iliyo Baringo zaidi ya mara kumi mwaka huu pekee anapoendelea kupenya maeneo tofauti kitaifa kwa kile kinachoonekana kuwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Uhasama kati ya Kanu na Jubilee katika Kaunti ya Baringo ulipamba moto hivi majuzi wakati Bw Moi alipompoteza mwandani wake kwa upande wa Bw Ruto kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Baringo Kusini.
Bw Charles Kamuren, ambaye aliwania ubunge eneo hilo kupitia KANU katika mwaka wa 2013, alihamia Chama cha Jubilee wakati wa hafla iliyohudhuriwa na Bw Ruto katika eneo la Marigat wiki mbili zilizopita.
Bw Kamuren sasa atawania ubunge wa Baringo Kusini kupitia Jubilee, huku KANU ikiamua hakitasimamisha mgombeaji yeyote. Uchaguzi huo umepangiwa kufanyika Agosti 17.
Wadhifa huo ulibaki wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge Grace Kipchoim miezi miwili iliyopita baada ya kuugua kwa muda mrefu.