• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Hatujafurushwa Orange House, tutaondoka Desemba – ODM

Hatujafurushwa Orange House, tutaondoka Desemba – ODM

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimekansha ripoti za vyombo vya habari kwamba kimefurushwa kutoka makao yake makuu ya Orange House, mtaa wa Kilimani, Nairobi.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa mawasiliano, Philip Etale, chama hicho kilisema kimekubaliana na mmiliki wa jumba hilo, Caroli Omondi, kwamba kiondoke kufikia Desemba mwaka huu.

“Tungependa kuthibitisha kwamba tutahama Orange House Desemba 31, 2018 mwaka huu kufuatia makubaliano kati yetu na mmiliko wake. Tumeafikiana kutoendelea kuwa wapangaji wa jengo hilo,” ikasema taarifa hiyo.

Hata hivyo, chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga hakikutaja mahala ambako kitahamishia makao yake makuu.

ODM imelitumia jumba la Orange tangu 2006, ambako kumeshuhudiwa rabsha hasa katika michujo kuelekea chaguzi kuu za 2007, 2013 na 2017 wagombeaji waking’ang’ania tiketi.

Bw Odinga pia hutumia jumba hilo kama mahala pa kuandaa mikutano muhimu kati yake na viongozi wa ODM kando na kuwa kitovu cha maandalizi ya chaguzi za mchujo.

Jana, gazeti moja la humu nchini liliripoti kwamba Bw Omondi, ambaye zamani alikuwa mwandani wa Bw Odinga, alikataa kuiruhusu ODM kuendelea kutumia jumba hilo akisema anataka kujenga jumba la kisasa katika ploti hiyo.

Bw Omondi, ambaye majuzi aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa mwanachama wa Bodi ya Shirika la Kitaifa la Mafuta (NOC), aliwahi kuhudumu katika cheo cha Mkuu wa Wafanyakazi katika Afisi ya Waziri Mkuu wakati Bw Odinga alipohudumu katika wadhifa huo kuanzia 2008 hadi 2013.

Hata hivyo, Bw Omondi alikosana na ODM mwaka jana alipodai kupokonywa ushindi katika mchujo wa kusaka tiketi ya kuwania kiti cha ubunge cha Suba Kusini dhidi ya Bw John Mbadi.

Mkurugenzi Mkuu wa ODM, Oduor Ong’wen alithibitisha kuwa watahamia mahala pengine.

mwishoni mwa mwaka huu kulingana na uamuzi wa baraza kuu la chama hicho uliofikiwa mnamo Mei mwaka huu.

“Ni kweli kwamba makao Makuu ya chama chetu yatahamishwa kutoka jumba la Orange hadi mahala pengine mwishoni mwa mwaka huu. Wanachama wetu, wafuasi na umma kwa jumla wataelezwa kuhusu mipango mingine ambayo itafuatia,” akasema Bw Ong’wen.

Bw Odinga, ambaye ni pia ni kiongozi wa muungano wa upinzani, NASA, amekuwa akitumia afisi zake za kibinafsi katika jumba la Capitol Hill, kama mahakala pa kukutana na wageni wake mashuhuri wakewemo mabalozi wa mataifa ya kigeni.

You can share this post!

Msako mkali Nakuru baada ya wakazi kulishwa paka

Pasta aliyeingia afisi ya Matiang’i bila idhini...

adminleo