• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
GIKOMBA: Wengi waliangamia wakiwa usingizini

GIKOMBA: Wengi waliangamia wakiwa usingizini

Na LUCY KILALO

WAATHIRIWA watano wa tukio la moto katika Soko la Gikomba walifariki Alhamisi wakipokea matibabu katika Hospitali Kuu ya Kenyatta.

Waathiriwa hao walikuwa miongoni mwa watu 70 waliojeruhiwa katika moto huo. Waliofariki ni watoto wanne, wote wa kike na mwanamke mmoja .

Kufikia jana mchana, zaidi ya watu 24 walikuwa wametibiwa kwa majeraha madogo ya moto, kuvuta moshi na pia mshtuko na kuruhusiwa kuondoka, huku 41 wakilazwa, watano miongoni mwao wakiwa hali mahututi.

Jamaa na marafiki walifika katika hospitali hiyo katika harakati za kutaka kujua hali ya wapendwa wao.,

“Wagonjwa watano wamepata majeraha ya moto ya zaidi ya asilimia 30 na wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ili wapate matibabu maalum. Wanne wana majeraha ya kuvunjika kwa miguu. Hospitali ya Kenyatta imefunguliwa na wagonjwa kulazwa humo katika wadi ya majanga ili waweze kushughulikiwa,” Kaimu afisa mkuu, Dkt Thomas Mutie alieleza.

Bi Betty Kaveke ambaye aliishi karibu na soko hilo alikuwa katika hospitali ya Kenyatta kujua hali ya wanawe.

“Sikuwa nyumbani moto ulipotokea na mwendo wa saa tisa usiku nilipigiwa simu kwamba kuna moto. Kufika hapo ambapo nilikuwa nimewaacha watoto wanne; wawili wangu na wawili wa dadangu, ni mmoja tu yule mkubwa ambaye alikuwa na fahamu,” alieleza akiwa anajiuliza maswali mengi kuhusu hali ya watoto hao wenye umri wa kati ya miaka miwili, minne na 14.

Alieleza pia kupoteza vitu vya nyumbani na hata Sh10,000 alizokuwa amepata katika biashara yake Jumatano, huku akiwa ameshikilia vipande kadhaa vya pesa hizo zilizochomeka.

“Yaani nilipofika mambo yalikuwa tu yamevurugika, ni kama kila mahali kumepukuliwa na maji yalijaa kila mahali,” alieleza.

Nao, Manusura Alice Kendagor, 25 na Charity Kemboi walikuwa wamelala waliposikia nduru za majirani. Kutoka walikumbana na moto kabla ya kukabiliana nao kujiokoa. Wawili hao walikuwa wakiishi katika nyumba moja.

“Nashukuru Mungu aliniokoa sikuumia sana. Tulikuwa kwa orofa ya tano,” alieleza Charity baada ya kutibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitali ya Kenyatta.

Wawili hao walikuwa na majeraha ya mkono na masikio na ni miongoni mwa waliotibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Dkt Mutie alieleza kuwa hospitali hiyo inafanya kila juhudi kuwasaidia waathiriwa na ilikuwa pia imetenga sehemu ya jamaa kuweza kupata maelezo kuhusu jamaa zao waliofikishwa hospitalini.

You can share this post!

GIKOMBA: Soko lenye historia ya mikasa ya moto

Muhoho abebe mzigo wake, Uhuru adinda kumtetea nduguye

adminleo