• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Hamtawahi kusikia wizi tena NYS, serikali yaahidi Wakenya

Hamtawahi kusikia wizi tena NYS, serikali yaahidi Wakenya

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imewahakikishia Wakenya kuwa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) halitakumbwa na kashfa nyingine baada ya uongozi mpya kuchukua usukani.

Waziri wa Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Profesa Margaret Kobia Jumatano alitoa hakikisho hilo alipomjulisha rasmi Mkurugenzi Mkuu mpya Bi Matilda Sakwa kwa Wakenya, katika hafla fupi iliyofanyika katika makao makuu ya shirika eneo la Ruaraka Nairobi.

Bi Sakwa ambaye kabla ya kuteuliwa kwake alikuwa Kamishna wa Kaunti ya Machakos anakuwa mahala pa Richard Ndubai ambaye mwezi Juni alikamtwa kuhusiana na sakata ya wizi wa Sh9 bilioni katika shirika hilo.

Bw Ndubai, ambaye alikamatwa pamoja na Katibu wa Wizara hiyo Bi Lilian Omollo, aliachiliwa kwa dhamana baada ya kuzuiliwa kuziuzini kwa mwezi mmoja.

“Kwanza ningependa kuomba msamaha kwa Wakenya kufuatia kutokea kwa sakata mbili katika NYS ambazo zimetoa picha mbaya kuhusiana na kazi tunayofanya hapo.

Kwa hivyo, tunaposimama hapa kumkaribisha Mkurugenzi Mkuu mpya ningependa kuwahakikishia Wakenya sakata nyingine sawa na hiyo haitatokea tena katika shirika hili,” Profesa Kobia akasema.

Aidha, Waziri huyo, ambaye aliteuliwa kusimamia wizara hiyo mapema mwaka huu, alisema chini ya uongozi wa Bi Sakwa pesa za NYS hazitafujwa wala kuibiwa, bali zitatumika kwa shughuli zilizokusudiwa.

Akaongeza: “Na madeni yote ambayo hayajalipwa ya kima cha Sh5.6 bilioni yaliyolimbikizwa kuanzia mwaka wa 20013 hadi 2017 hayatalipwa. Tunataka kuendesha uchunguzi kubaini uhalali ya madeni hayo, ili kuzuia visa vya malipo kutolewa kwa wafanyabiashara walaghai.”

Akiongea katika hafla hiyo, Bi Sakwa aliwaomba Wakenya kumpa muda ili aweze kujifahamisha na majukumu ya afisi yake katika wadhifa wake mpya.

Hata hivyo, aliihakikishia serikali kuwa atafanya kila awezalo ili kuleta mabadiliko katika shirika hilo kanda na “kuleta uthabiti katika usimamizi wa rasimali zake zote.

“Kwa hivyo, nawaomba Wakenya na wafanyakazi wote wa NYS kuniunga mkono ili niweze kufanyakazi kwa manufaa ya wote.”

You can share this post!

Mbona KDF wasiondolewe Somalia? ashangaa mbunge

Hakuna atakayesazwa katika vita dhidi ya ufisadi – PAC

adminleo