• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
Wakazi wa Kogelo watamauka kuzuiwa kuhudhuria hotuba ya Obama

Wakazi wa Kogelo watamauka kuzuiwa kuhudhuria hotuba ya Obama

Na WANDERI KAMAU

WAKAZI wa kijiji cha Kogelo, Kaunti ya Siaya Jumatatu walipigwa na butwaa baada ya kukosa kuhutubiwa na aliyekuwa rais wa Amerika, Barack Obama.

Licha ya msisimko mkubwa waliokuwa nao kutokana na ziara yake, wakazi walizuiwa kuingia katika Kituo cha Michezo cha Vijana cha Sauti Kuu, ambacho Bw Obama alizindua. Wengi walilazimika kufuatilia hotuba yake kwa umbali.

Hali ya usalama ilikuwa kali na baadhi walibishana na maafisa wa usalama. Gavana wa Siaya, Cornell Rasanga alijipata pabaya baada ya hali ya mtafaruku kuzuka kati yake na maafisa wa usalama waliokuwa katika lango kuu la kuingia kituoni humo.

Bw Rasanga alikataa kukaguliwa, akisisitiza kuwa huko ni kumkosea heshima kama kiongozi wa kaunti hiyo. Gavana huyo alitishia kurudi nyumbani, ikiwa walinzi hao wangesisitiza kumkagua.

“Huku ni sawa na kunikosea heshima. Nitarudi nyumbani, kwani hilo ni sawa na kunidhalilisha,” akalalama Rasanga.

Hali ilikiwa sawa kwa Gavana wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o, ambaye alilazimika kutii amri ya walinzi hao na kukubali kukaguliwa kama wananchi wengine. Prof Nyong’o alipanga foleni na wageni wengine waliokuwa wamealikwa.

Kama hilo halikutosha, ni watu wachache pekee ambao waliruhusiwa kuingia nyumbani kwa Mama Sarah Obama, ambako Bw Obama alizuru kwa muda mfupi, kabla ya kuondoka kwenda Afrika Kusini.

Wengi waliotarajia kwamba angaa angewahutubia kama waliachwa hoi baada ya kufahamu kuwa Bw Obama alikuwa ashaondoka, na hangepata nafasi ya kuwazungmzia.

Lakini kwenye hotuba yake, Bw Obama alieleza kuunga mkono mwafaka wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.

Vile vile alieleza kuunga mkono vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi nchini.

Alisifu mwafaka huo, akiutaja kuwa nafasi kuu kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga kushughulikia changamoto ambazo zinawakumba mamilioni ya Wakenya.

“Mazingira ya utulivu wa kisiasa uliopo kwa sasa yanapaswa kutoa nafasi kwa viongozi hao wawili kushughulikia changamoto za kimsingi kama ufisadi, uhasama wa kikabila na hali za umaskini ambazo bado zinawaandama Wakenya,” akasema.

Kauli yake ilijiri huku vita dhidi ya ufisadi vikiwa vimeshika kasi nchini. Miongoni mwa sakata zinazochunguzwa kwa sasa ni madai ya wizi wa fedha katika Shirika la Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS) na Shirika la Umeme Kenya (KP).

Hata hivyo, alieleza imani yake kuhusu ustawi wa kisiasa na kijamii, kwani katiba ya sasa inatoa nafasi kwa ushughulikiaji wa changamoto zinazoikumba nchi.

You can share this post!

Faini ya Sh40,000 kwa kuvuta shisha

Kuria akaangwa kusema Obama alitoa hotuba ya kudhalilisha...

adminleo