Habari Mseto

Muthama na Aladwa waomba kesi zao zitamatishwe

July 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Makadara George Aladwa na aliyekuwa Seneta wa Machakos Bw Johnstone Jumatano walidokeza wameandikia Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) itamatishe kesi za ufisadi dhidi yao.

Wakili Dkt John Khaminwa alimweleza hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi  kuwa ameandikia NCIC barua itamatishe kesi za uenezaji chuki na uhasama wa kikabila dhidi yake Mabw Aladwa na Bw Muthama.

Dkr Khaminwa alimweleza Bw Andayi kwamba washtakiwa wameomba NCIC itamatishe kesi dhidi yao kufuatia ushirikiano mpya kati ya kinara wa upinzani Bw Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka ya kueneza chuki baina ya makabila mbali mbali .

Bw Aladwa anadaiwa alitamka maneno ya uchochezi kwa kusema kuwa “ lazima watu kadhaa wafe ndipo Bw Odinga achaguliwe kuwa rais.”

Bw Muthama anadaiwa alitumia lugha ya kumdunisha Rais Kenyatta kwa kumtaka wakutane katika bustani ya Uhuru Park bila walinzi wake akiandamana na naibu wake William Ruto wachapane Makonde itambuliwe nani yuko nguvu kuliko mwingine.

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP aliomba muda awasiliane na NCIC kubaini ikiwa kesi dhidi ya wawili hawa itaondolewa au la.

Kesi itatajwa Novemba 29 2018. Mabw Aladwa na Muthama wamekanusha mashtaka dhidi yao na wako nje kwa dhamana.