• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Muthoni na Kindiki waitwa na Njuri Ncheke

Muthoni na Kindiki waitwa na Njuri Ncheke

Na Alex Njeru

BARAZA la Wazee la Ameru, Njuri Ncheke limewaita Gavana Muthomi Njuki (Tharaka Nithi) naibu wake Nyamu Kagwima na Seneta Kindiki Kithure kwa kikao cha dharura ili kuelezea kiini cha tofauti zao.

Wakiwahutubia wanahabari jana katika soko la Kathwana, baada ya kukutana kwa saa kadhaa, wazee hao walisema kwamba viongozi hao wanapaswa kufika mbele yao mnamo Agosti 13, 2018.

Waliongozwa na mwenyekiti wa baraza hilo katika kaunti ya Tharaka Nithi, Bw Kangori M’Thaara.

“Viongozi hao watatu, Gavana Njuki, naibu wake, Bw Kagwima na Seneta Kindiki wameagizwa kufika mbele ya baraza hilo ili kueleza sababu ya mgawanyiko wao,” akasema Bw Kangori.

Mwenyekiti huyo alieleza kwamba viongozi hao, ambao vilevile ni wanachama wa baraza hilo wanatarajiwa kufika binafsi siku hiyo, kwenye kikao kiakachoandaliwa mjini Kathwana.

Alisema kuwa ni sikitiko kwa viongozi hao kutofautiana hadharani, licha ya kuripoti masuala hayo kwa wazee.

“Tumemsikia gavana na naibu wake wakitofautiana hadharani kuhusu bajeti ya 2018/2019. Cha kushangaza zaidi ni kwamba waliwasilisha masuala hayo kwa vyombo vya habari, hata kabla ya kuwaarifu wazee,” akasema.

Kwa hayo, alisema kuwa wazee hawajafurahishwa na uhusiano kati ya Prof Kindiki na Gavana Njuki, waliosema kwamba umeendelea kudorora tangu uchaguzi wa Agosti 8.

Bw M’Thaara alisema kwamba Bw Njuki na Prof Kindiki huwa wanajifanya hawana tofauti hadharani, ila wameambiwa kwamba kuna tofauti kubwa sana kati yao.

Katibu wa baraza hilo Abraham Mati na naibu wake Muthei Kiongo, walisema kuwa tofauti kati ya viongozi hao zimeathiri maendeleo na hali ya mshikamano katika kaunti hiyo.

Kwa upande wake, Bw Kiongo alisema kuwa baraza hilo halitawavumilia viongozi ambao wanazua migawanyiko. Walionya kuwa huenda wakawalaani.

You can share this post!

Wazee wa Agikuyu wamkataa Ngunjiri kuwa msemaji wa jamii

Aibu machifu kuwalinda wanajisi

adminleo