• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 3:17 PM
Kalonzo aonya Uhuru kuhusu wandani wake

Kalonzo aonya Uhuru kuhusu wandani wake

Na VALENTINE OBARA

JUHUDI za Rais Uhuru Kenyatta kupambana na ufisadi ziko hatarini kuhujumiwa na wandani wake, Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameonya.

Akizungumza alipokutana na Wakenya wanaoishi Uingereza, Bw Musyoka alisema kwamba anaunga mkono juhudi hizo za rais lakini akamtahadharisha kuhusu wandani wake ambao wamejitolea mhanga kuzivuruga.

“Rais Uhuru Kenyatta ana nia njema katika jitihada zake za kuangamiza ufisadi nchini Kenya lakini kuna watu wenye mamlaka makubwa ambao ni vizingiti na wanaweza kuhatarisha sana lengo lake,” akasema.

Kwa miezi kadhaa sasa, maafisa wa mashirika mbalimbali ya serikali wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kushtakiwa kwa madai ya kuhusika katika ufisadi.

Mashirika hayo yanayojumuisha Kenya Power na shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) yamedaiwa kukumbwa na ufujaji wa mamilioni ya pesa za umma.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa hasa kutoka maeneo ya Rift Valley, wamekuwa wakilalamika wakidai kwamba juhudi hizo zinalenga kuhujumu azimio la Naibu Rais William Ruto kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanywa 2022.

“Natumai rais atasimama kidete na kulenga ruwaza yake ya kuangamiza ufisadi nchini. Kenya iko katika njiapanda na inahitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu kukabiliana na ufisadi uliokithiri na kupunguza madeni makubwa ya taifa,” akasema Bw Musyoka.

Akizungumza Jumapili alipokuwa katika Kaunti ya Kilifi, Bw Ruto alitaka wanasiasa wote washirikiane kutatua changamoto zinazokumba wananchi bila kuingiza siasa katika juhudi zinazoendelezwa.

Alitaka viongozi wajiepushe na uchochezi wa kisiasa kwani unaathiri maendeleo ya wananchi, na kuwakumbusha kuwa kipindi cha uchaguzi kilikamilika mwaka uliopita.

“Ninawaomba viongozi wenzangu wote waliochaguliwa, nafasi tuliyonayo si ya kuchochea uhasama bali kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazotukumba. Ni lazima tutafute suluhisho kwa njia yenye heshima,” akasema naibu rais.

Akiwa Uingereza, Bw Musyoka alizindua tawi la Chama cha Wiper katika jiji la Birmingham.

Alirejelea kauli kuwa anaunga mkono muafaka kati ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga kwani unalenga kuleta umoja wa Wakenya na maendeleo nchini.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema kwamba chama chake kinaendeleza mikakati ya kutafuta ushirikiano na vyama mbalimbali kwa maandalizi ya uchaguzi wa 2022.

Katika ziara hiyo, aliandamana na Kaimu Mwenyekiti wa Wiper, Bw Patrick Kiilu, Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Makueni, Bi Rose Mumo Museo na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Kennedy Musyoka.

You can share this post!

Walimu waonywa dhidi ya kuuza sodo za serikali

Ashtakiwa kulangua wasichana wa kigeni

adminleo