Aliyeibia mamaye aponde raha na mchumba asukumwa ndani

Na RICHARD MUNGUTI

MWANACHUO aliyeiba pesa za mama yake kuzitumia  akiwa na mpenziwe kuponda raha ameamriwa awekwe chini ya uangalizi wa maafisa wa urekebishaji tabia baada ya mahakama kuambiwa imfunge jela apate adabu.

Akiamuru ripoti ya urekebishaji tabia iwasilishwe kortini , hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi alishangaa sababu ya mama yake  Bi Cynthia Cherop kumchukia kiasi cha “ kutaka afungwe jela.”

Bw Andayi alimwuliza Cherop, “Bali na kuiba pesa za mama yako mtumie na mpenzi wako  Josephat Ng’ang’a, ni kitu gani kingine ulimfanyia mama yako hata akakuchukia na kutaka utokomee machoni mwake?”

Hakimu aliuliza ikiwa mama yake mwanafunzi huyo wa chuo kikuu Bi Milkah Sitati  amefika kortini kujua hatma ya bintiye.

“Mama yako amefika kortini leo kujua ikiwa utafungwa ama kuachiliwa,” Bw Andayi alimwuliza mshtakiwa.

“Hapana hakufika kortini leo. Aliniambia yeye ni mtumishi wa umma na anaogopa kupigwa picha za televisheni na za kuchapisha kwa magazeti,” kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alijibu.

“Hata sisi  ni watumishi wa umma na kila siku tunapigwa picha,” Bw Andayi alimweleza Bw Naulikha.

Wajomba wawili wa mshtakiwa walisimama kortini na kuomba mahakama iwakabidhi mshtakiwa awe akiishi kwao muda atakapokuwa chuoni.

Wajomba hao walimweleza hakimu dada yao hataki tena kuishi na bintiye kwa “ vile amemaibisha”

“Siwezi kumkabidhi mshtakiwa watu ambao siwajui. Nitamtuma afisa wa urekebishaji tabia akamhoji mama yake msichana huyu mwenye umri wa miaka 21 aeleze sababu ya kumchukia bintiye,” Bw Andayi aliwaeleza wajomba hao.

Mshtakiwa alimweleza hakimu kuwa anataka kuendelea na masomo ijapokuwa mamayake amemchukia.

Akijitetea mshtakiwa aliomba msamaha akisema , “ ameghairi kumkosea mama yake kwa kuiba kadi zake za benki za Barclays na National ambapo alitoa jumla ya Sh70,000 akiwa na rafikiye Josephat.”

Mahakama iliambiwa kamera za CCTV katika benki ya Barclays ziliwanasa wawili hao Cherop na Josephat wakichukua pesa kutoka kwa akaunti.

Bw Andayi aliambiwa kadi mbili za akaunti za BI Milkah Sitati hazijapatikana.

Mshtakiwa aliamriwa azuiliwe katika gereza la Langata hadi Agosti 1, 2018 ripoti ya urekebishaji tabia itakapotolewa.

Bi Cherop alikiri mashtaka manne ya kufanya njama za kumwibia mama yake na kuiba Sh70,000 kutoka kwa akaunti za mama yake zilizo  katika Benki za Barclays na National Juni 4, 2018.

Habari zinazohusiana na hii

NDIO! HAPA WIZI TU